Zuchu: Babu Tale, Fela walinikataa

Muktasari:

Said Fella na Tale ni miongoni mwa vigogo kwenye lebo ya WCB inayowamiliki Diamond Platnumz.

HABARI ya mjini kwa sasa ni kuteka game ya Bongo Fleva kwa supastaa wa kike, Zuhura Othman a.k.a Zuchu.
Zuchu, ambaye ni mtoto wa malkia wa taarabu nchini, Khadija Omary Kopa, ndio anatesa kwa sasa akiiweka juu WCB kama ilivyokuwa na wasanii wengine wa lebo hiyo akiwemo Rayvanny, Mbosso na Lavalava.
Hata hivyo, safari ya Zuchu hadi kufikia kuisimamisha Bongo akitesa na ngoma zake kibao ikiwemo Cheche aliyopiga kolabo na Diamond mwenyewe, amepitia milima na mabonde ikiwemo kukataliwa mchana kweupee.
Ndio, Zuchu amezungumza na timu ya burudani ya Mwanaspoti na kufichua mambo kibao ikiwemo kukataliwa na mameneja wa WCB, Said Fella na Babu Tale.
Zuchu amefichua kuwa miaka michache iliyopita akiwa bado mwanafunzi alitia timu kwenye ofisi za WCB kuomba wampe nafasi ya kuonyesha kipaji.
“Nilipofika WCB na kukutana na Babu Tale aliniangalia kisha akaniambia nirudi shule kuendelea na masomo na muda ukifika naweza kurudi wakanifikiria kunichukua,” anasema Zuchu.
Hata hivyo, jibu hilo halikumfanya kuwa mnyonge na badala yake akabadili upepo kwenda kwa Fella, ambaye anamiliki kituo cha Mkubwa na Wanawe kule TMK.
“Niliondoka WCB na kuamini bahati yangu inaweza kuwa kwa Mkubwa na Wanawe, lakini nako nilipofika majibu hayakuwa na tofauti sana. Fella aliniambia bado ni mdogo na kunishauri niendelee na shule kwanza,” anaongeza Zuchu.
Miaka minne baada ya kumaliza stashahada ya uchumi kule India, aliamua kuingia kwa kishindo kwenye game akianza kwa kurudi WCB ambapo alifanyiwa usaili mara mbili kujiridhisha na kipaji chake.
“Mabosi zangu waniambia kuwa hawataki kunichukua katika lebo kwa sababu tu ni mtoto wa Hadija (Kopa), bali wanataka mtu mwenye kipaji cha ukweli na anayeweza kusimama mwenyewe. Nikapewa mtihani wa kutunga wimbo pale pale. Mara ya kwanza haukuwa mzuri, nikarudia tena kwa kupewa biti mbalimbali na hapo ndio nikatunga versi ya Wana. Nashukuru ndio umekuwa wimbo wangu wa kwanza na umefanya vizuri baada ya kutangazwa na WCB na umefungua neema kwangu,” amesema Zuchu.

Pata mahojiano kamili ya Zuchu ndani ya Jarida la Starehe Jumamosi ya Septemba 19, 2020 na ndani ya Jarida la Weekend Vibe ndani ya Mwanaspoti, Jumapili ya Septemba 20, 2020. Pia, tembelea Youtube ya Mwananchi Digital kuona laivu mahojiano yake.