Mtibwa Sugar yaiporomosha Simba, Yanga

BAO pekee lililofungwa na mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Jaffary Kibaya lilitosha kuipa pointi tatu timu hiyo ambayo tangu Ligi Kuu kuanza metoka sare mechi zake zote mbili.
Mtibwa Sugar walitoka sare tasa dhidi ya Ruvu Shooting huku sare nyingine ya bao 1-1 wakiipata dhidi ya Simba, mechi iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Kibaya aliipatia bao Mtibwa Sugar dakika ya 35 kipindi cha kwanza bao ambalo lilidumu hadi dakika 90 za mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Hii ni mechi ya raundi ya tatu kwa timu zote hizo, ambapo Ihefu imecheza mechi zote nyumbani na kushinda moja tu dhidi ya JKT Tanzania bao 1-0, huku ikifungwa na Simba bao 2-1 pamoja na Mtibwa Sugar.
Kwa matokeo hayo, Mtibwa Sugar imekusanya pointi tano ikipanda hadi nafasi ya tano ikiishusha Simba na Yanga zenye pointi nne kila moja wakati Ihefu imeporomoka mpaka nafasi ya 11.
Akizungumza mara baada ya mechi hiyo kocha wa Ihefu FC, Maka Mwalwisi amesema; "Kuchezea mpira ndiyo falsafa yetu na hatutabadilisha, tumepata nafasi hatujazitumia vizuri, tunaamini tutapata pointi ugenini kama wengine walivyopata hapa kwetu,".
Upande wa kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amesema; "Nafurahi tumepambana tumepata pointi tatu ugenini, nimefurahishwa na maingizo mapya kwenye kikosi changu ingawa hawajafikia kwenye ubora ninaoutaka ndiyo maana nimekuwa nikibadilisha kikosi,".