Ihefu, JKT Tz, Polisi zatamba kusaka pointi

Muktasari:

Mechi za mzunguko wa tatu zaanza kupigwa leo, Wajeda watambiana.

LIGI Kuu Bara inaendelea leo Ijumaa Septemba 18, 2020 kwa kukutanisha mechi mbili katika viwanja viwili tofauti, Uwanja wa Ushirika mjini Moshi na Sokoine jijini Mbeya ikiwa ni mechi za raundi ya tatu.
Polisi Tanzania ndio watakuwa wenyeji katika Uwanja wa Ushirika saa 8:00 mchana wakiwakaribisha JKT Tanzania huku Ihefu wao wakiwa nyumbani wakicheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mchezo wa Polisi Tanzania na JKT Tanzania utakuwa mkali kutokana na timu zote mbili kuwa na pointi sawa (pointi tatu) huku kila mmoja akiwa amecheza michezo miwili.
Kwa upande wa Ihefu wao wanashika nafasi ya saba wakiwa na pointi tatu huku wakicheza na Mtibwa Sugar wanaoshika nafasi ya 11 wakiwa na pointi mbili, mchezo huu utakuwa na upinzani mkubwa kwani Mtibwa watahitaji matokeo na kujiondoa  kwenye nafasi hiyo.

Kesho Jumamosi pia kutakuwa na kibarua kigumu kati ya Kagera Sugar dhidi ya Yanga mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba, huku Prisons wao wakiwakaribisha Namungo katika Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.


MAKOCHA WAFUNGUKA
Kocha wa Ihefu, Maka Mwalwisi amesema wataingia katika mchezo huo wakitumia akili sana kwani Mtibwa Sugar ni moja ya timu yenye wachezaji wenye vipaji.
"Tuko kamili kuelekea mchezo huo ambao naamini utakuwa mgumu kutokana na aina ya timu tunayokutana nayo.Tutaikabili Mtibwa kwa akili na ufundi mwingi kwa sababu ni moja ya timu ngumu inayocheza mpira mzuri", amesema Mwalwisi.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema wanaiheshimu Ihefu kwani ni timu nzuri hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari kubwa.
"Hatuwezi kuidharau Ihefu kwani ni timu nzuri na ndio maana iko kwenye ligi. Tutacheza kwa tahadhari ili kuhakikisha tunapata pointi tatu", amesema Katwila.
Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed 'Bares' amesema kuwa watapambana kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.
"Mechi iliyopita tulipoteza hivyo hatutaki kuona tunapoteza mechi nyingine.Tunajua tunakutana na timu ngumu ya Polisi ambayo mchezo uliopita walishinda hivyo watatukabili wakiwa ana ari kubwa lakini hata sisi tumejipanga hivyo ni jambo la kusubiri kuona", amesema Bares.
Naye kocha wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini amesema wamejipanga vizuri kushinda mchezo huo na wanaamini wataondoka na pointi tatu ili kuwaonyesha JKT Tanzania kuwa wao ni wakubwa zaidi yao.
"Ni mechi ya dabi hiyo lazima tupambane ili tushinde na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.Tunawaheshimu JKT Tanzania lakini  lazima tuwafunge', amesema Malale.