Kocha Mbao aiota Ligi Kuu

WAKATI Mbao FC ikitarajia kuingia kambini leo Jumatatu kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Kocha wa timu hiyo, Almasi Moshi amesema malengo yao ni kurudi haraka Ligi Kuu kutokana na usajili walioufanya.

Mbao ilishiriki Ligi Kuu kwa misimu minne mfululizo, ilishuka daraja msimu uliopita na sasa itaanza kutafuta tiketi ya kupanda Oktoba 3 mwaka huu.

Kocha huyo ambaye alikuwa msaidizi wa Fred Felix ‘Minziro’ aliongeza anajivunia usajili mkubwa wa wachezaji wenye uwezo na uzoefu, pia ambao wanahitaji kufanikiwa.

“Tunaanza rasmi mazoezi ya pamoja kesho (leo) Jumatatu na matarajio yetu ni kuirudisha timu Ligi Kuu, tumefanya usajili mchanganyiko wapo waliocheza Ligi Kuu, FDL na ambao wanasaka majina,” alisema Moshi.

Alisema baada ya kuingia kambini ataanza kutengeneza muunganiko ili ligi itakapoanza awe na kikosi bora chenye kushinda kila mechi na kupanda daraja mapema.

Kocha huyo alisema pamoja na matarajio makubwa kwao msimu ujao, lakini hawatadharau timu yeyote isipokuwa watapambana kuhakikisha wanafikia malengo.