Bodi yadhibiti mashabiki kuingia bure kwa Mkapa

Muktasari:

Mashindano ya riadha taifa bado yanaendelea kwa michezo ya fainali za mbio fupi na miruko ambayo inatarajiwa kuanza saa 8 mchana.

BODI ya Ligi nchini (TPLB) maarufu kama Steward imelazimika kuweka ulinzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia asubuhi leo Jumapili  ili kuzuia mashabiki kufanya udanganyifu kwa kuingia bure kutizama mechi dhidi ya Mbeya City itakayoanza saa 1:00 usiku  kwa kisingizio cha kwenda kuangalia mashindano ya riadha Taifa.

Mechi ya Yanga itasubiri hadi kumalizika mashindano ya riadha Taifa ambayo yanatarajiwa kufungwa saa 11 jioni ili kuanza kuingia uwanjani kutizama mechi hiyo ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara.
Jana Jumamosi, kulikuwa na sintofahamu ya mechi hiyo kama itachezwa Uwanja wa Mkapa au lah kutokana na ratiba za riadha kutarajiwa kumalizika saa 12 jioni, saa moja kabla ya muda wa mechi hiyo.
"Tutamaliza saa 11 jioni, hivyo baada ya muda huo wao wataendelea na programu zao, ingawa inategemea na namna hafla ya kufunga itakavyokwenda, tunaweza kumaliza ratiba yetu saa 12 jioni au hata saa moja," amesema Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi.
Yanga ambayo italazimika kusubiri hadi muda wa mashindano ya riadha kumalizika ndipo waingie uwanjani, ambapo bodi imelazimika kulinda uwanja huo tangu saa 4 asubuhi ili kuzuia baadhi ya mashabiki kutumia kigezo cha riadha kuingia bure uwanjani.
Licha ya tiketi kuendelea kukatwa uwanjani hapo, walinzi hao wamekuwa mbogo kwa watu ambao wanawatilia shaka kuwa si wanariadha kuingia uwanjani hapo mapema.
MCL Digital imewashuhudia baadhi ya watu wakirudishwa kuingia uwanjani hapo na kutakiwa kukaa mbali na mageti ya kuingilia uwanja huo hadi watakapotoa muda rasmi wa kuanza kuingia uwanjani.