Ni Yanga, Mbeya City leo, Mtibwa yaikomalia Simba

Muktasari:

Yanga itaikaribisha Mbeya City leo katika mchezo wa Ligi Kuu ambao hadi jana jioni ulikuwa na hatihati ya kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa kutokana na kutumika kwa mashindano ya riadha ngazi ya Taifa.

Dar/Moro. Yanga itaikaribisha Mbeya City leo katika mchezo wa Ligi Kuu ambao hadi jana jioni ulikuwa na hatihati ya kufanyika kwenye Uwanja wa Mkapa kutokana na kutumika kwa mashindano ya riadha ngazi ya Taifa.

Mchezo huo umepangwa kuanza saa 1:00 usiku, lakini mashindano ya riadha yaliyoanza jana uwanjani hapo ni kama yanataka kutibua jambo.

Inadaiwa baadhi ya viongozi wa Yanga wakiongozwa na mkurugenzi wa mashindano wa klabu hiyo, Thabeet Kandoro walifika kwenye Uwanja wa Mkapa jana kufanya mazungumzo na wale wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ili kuweka mambo sawa.

Thabeet alisema mechi hiyo itachezwa saa 1:00 usiku kwenye uwanja huo, licha ya uongozi wa RT kudai ratiba yao itakwenda hadi saa 12 jioni.

Alisema kama riadha itamalizika saa 11 jioni uhakika wa mechi kuanza saa 1:00 usiku utakuwepo.

Kuhusu kuhamishia mechi hiyo Uwanja wa Uhuru au kuisogeza mbele hadi saa 3 usiku, alisema haiwezekani kwani itaathiri mapato yao.

“Labda iaharishwe tu isichezwe kesho (leo), jambo ambalo pia haliwezekani, tumewaomba riadha wajitahidi angalau wamalize saa 11 jioni, muda huo utakuwa rafiki kwa mechi yetu kuanza saa moja usiku kama ilivyopangwa,” alisema Thabeet

Katibu wa TOC ambao ndio wanaratibu riadha kwa kushirikiana na RT, Filbert Bayi alisema ratiba yao itakwenda hadi saa 12 jioni. “Yanga wasitupangie muda wa kumaliza, tutaondoka uwanjani saa 12 jioni baada ya ratiba kukamilika na si vinginevyo,” alisema.

Meneja wa Uwanja wa Mkapa, Nsajigwa alisema wanatarajia ratiba ya riadha itamalizika mapema.
“Walishazungumza Yanga na watu wa riadha hilo suala, kama riadha watamaliza saa 11 jioni haitaathiri mechi ya Yanga usiku,” alisema Nsajigwa.

Kazi ipo

Hapana shaka sare ambayo Yanga walipata katika mchezo wa kwanza dhidi ya Prisons itachochea kuingia kwa nguvu kuivaa Mbeya City katika mchezo huo. Mbeya City ambayo mchezo wa kwanza ilikubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa KMC huenda ikajitutumua kusahihisha kosa na hivyo mchezo huo kuufanya kuwa mtamu.

Hata hivyo rekodi zinaibeba Yanga dhidi ya Mbeya City kwani imekuwa ikipata matokeo mazuri kila inapoikabili timu hiyo jijini Dar es Salaam. Tangu Mbeya City ipande daraja kucheza Ligi Kuu 2013, imekutana na Yanga mara saba jijini humo.

Katika mechi hizo, Yanga imeshinda mara sita na kupata sare moja.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema wamejiandaa vizuri kuchukua pointi zote tatu.

Simba, Mtibwa hakuna mbabe

Bingwa wa Ligi Kuu, Simba SC jana ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji wao, Mtibwa Sugar katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mzamiru Yassin ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao kwa Simba katika dakika ya 45 kwa shuti kali akimalizia pasi ya Clatous Chama.

Timu hizo zilienda mapumziko Simba ikiongoza kwa bao hilo, lakini dakika moja tangu zirejee kipindi cha pili Mtibwa Sugar ilisawazisha kwa bao lililofungwa na Boban Zirintusa kwa kichwa akimalizia krosi ya Issa Rashid.

(Imeandikwa na Olipa Assa - Morogoro, Oliver Albert na Imani Makongoro-Dar)