Straika Gor Mahia asaini Dodoma Jiji

Friday August 14 2020

 

STRAIKA Dickson Ambundo aliyekuwa anaichezea Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu Kenya, amejiunga na Dodoma Jiji kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Meneja wa mchezaji huyo, Ally Mohammed ameiambia Mwanaspoti Online leo Ijumaa Agosti 14, 2020 kuwa Ambundo alikuwa na ofa nyingine ya Polisi Tanzania lakini viongozi wa timu hiyo ni kama walikuwa wanajivuta.

"Ambundo amesaini muda mchache uliopita mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kukubaliana kila kitu na ndio maana amesaini,".

"Polisi Tanzania walimuhitaji lakini baadaye wakawa kimya mpaka hivi leo aliposaini Dodoma Jiji," amesema Meneja wake huyo.

Mpaka sasa Dodoma Jiji imesajili nyota nane pamoja na Ambundo ukichana na wale wa zamani walioipandisha timu na kuongezwa mikataba mipya.

Wengine ni Cleophance Mkandala (Prisons), Peter Mapunda na Aron Kalambo (Mbeya City), Michael Chinedu (Alliance), Seif Karie (Lipuli), Jukumu Kibanda (Namungo), Justine Omary (Biashara United) na Augustino Ngata (Mwadui FC).

Advertisement

Advertisement