Real Madrid yang'oka, Juve presha tupu kwa CR7

Muktasari:

Tangu mwaka 2010, hii ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji wa Kireno, Ronaldo chama ambalo analichezea  kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya 16 bora.

TURIN, ITALIA

KIMENUKA huko Turin, unaambiwa baada ya Juventus kufungashiwa virago vyao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kanuni ya bao la ugenini viongozi wa Juventus wameingiwa na wasi wasi kuwa huenda wakampoteza nyota wao, Cristiano Ronaldo, huku Real Madrid nayo iking'olewa kibabe.

Licha ya Ronaldo kutupia mabao mawili usiku wa jana kwa upande wa Juventus hayakutosha kuwafanya kutinga hatua ya robo fainali kutokana kuruhusu kwao bao moja kwenye mchezo huo lililoipa faida Lyon ya kikanuni na kusonga mbele.

Katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa nchini Ufaransa, Lyon waliisapraizi Juventus ya Ronaldo wao kwa kuwafunga bao 1-0 hivyo walikuwa na mtaji wa bao hilo kwenye mchezo wa marudiano.

Mwenyekiti wa Juventus, Andrea Agnelli amesema watajaribu kumshawishi Ronaldo ambaye amekuwa akihusishwa kutimkia nchini Ufaransa kwenye klabu ya PSG, kuendelea kusalia.

"Ninauhakika kabisa abaki," Agnelli ameimbia Sky Sport Italia.

''Nadhani ripoti hiyo kuwa anaweza kuondoka ilikuwa  miezi kadhaa iliyopita, ambayo ilichapishwa tu kabla hatujacheza dhidi ya timu ya Ufaransa. Ni hila ya vyombo vya habari.

"Hapana, ninaweza kukuhakikishia Ronaldo atabaki kuendelea kuwa nguzo ya Juventus,” amesema.

Wakati Juventus wakitupwa nje ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya, Real Madrid nao walikiona chamoto huko Manchester, England kwa kukumbana na kipigo cha mabao 2-1.

Matokeo hayo, yameifanya Manchester City kutinga katika hatua ya robo fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2 katika hatua hiyo wanatarajiwa kukutana na Lyon, Agosti 15.

Michezo mingine ya Ligi ya Mabingwa inatarajiwa kuchezwa leo ambapo Chelsea watakuwa na mlima mkubwa wa kupamba wa mabao 3-0 dhidi ya Beyern Munich, Barcelona watacheza dhidi ya Napoli.