Mzee Yusuf nusura ahairishe mambo

WAKATI mkewe Leyla Rashid akieleza alivyoamua kupambana na maneno na kebehi za watu, baada ya Mzee Yusuf kurejea kwenye muziki, mumewe huyo kwake imekuwa tofauti akifuchua ilibaki kidogo tu ahirishe uamuzi wake wa kurejea kwenye miondoko ya taarabu alikopumzika kwa miaka kama minne.

Mtunzi na mwimbaji huyo anayejulikana kama Mfalme wa miondoko hiyo,  alitangaza kuacha kuimba mwaka 2016 na kujikita katika shughuli za ualimu wa dini na kutoa da'wa, haata hivyo Machi 12 alipowashtua wengi alipoandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa anarudi mjini na ataimba mpaka agaregare.

Katika kutimiza ahadi hiyo usiku wa jana Ijumaa (Agosti 7, 2020) katika ukumbi uliopo Mbagala, jijini Dar es Salaa Mzee amefanya onyesho lake la kwanza alilolipa jina la 'Mzee Yussuf Narudi Mjini' na kufunika kinoma kwa mashabiki kuonekana kupagawa naye baada ya kumkosa kwa muda mrefu.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, lililotaka kujua namna gani alivyopokea maoni ya watu baada ya kutangaza kurejea kwenye muziki, amesema alikuwa anaumia na ilifika mahali akataka kuahirisha.

"Asikuambia mtu, maneno wanayotoa watu mitandaoni dhidi yangu yananiumiza mno, mpaka ilifika mahali nikasema sijui niahirishe, lakini nikarudi nyuma na kufikiria yanayonisibu na familia yangu nikaona bora kusonga mbele," amesema Mzee Yusuf bila kufafanua yapi yalityomsibu na kuongeza;

"Kwani kesho na keshokutwa nikija kuharibiwa ni hawa hawa watakuja kunicheka, kikubwa bado namwamini Mungu wangu na hii ni njia tu katika kutafuta rizki," amesema Mzee Yusuf.

Kuhusu mipango yake ya baadaye, amesema wanatarajia kuja na kundi na huenda likawa lilelile la Jahazi kama maongezi na waliokuwa wakilisimamia yataenda vizuri na ikishindikana basi wataanzisha jingine.