Messi anasepa? acheni utani nyie

Muktasari:

Inter Milan imekuwa klabu inayotajwa sana kwamba, inaweza kumng’oa Messi ndani ya Barca, hasa wakati huu ambao kunaonekana kuwepo kwa msuguano mkubwa kati ya nahodha huyo na baadhi ya mabosi zake.

BARCELONA, HISPANIA

MASHABIKI wa Barcelona wametakiwa kuendelea kulala usingizi mzuri na kupuuza taarifa zote kuhusu supastaa wao, Lionel Messi.

Baadhi ya mashabiki wa Barcelona walikuja juu baada ya kuzagaa taarifa kwamba, Messi anaweza kuachana na wababe hao wa Catalan baada ya kumaliza mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, Rais wa Barcelona, Josep Bartomeu akaibuka na kuwataka mashabiki kuondoa hofu kwani, Messi amemweleza atastaafu soka akiwa ndani ya jezi ya klabu hiyo.

Inter Milan imekuwa klabu inayotajwa sana kwamba, inaweza kumng’oa Messi ndani ya Barca, hasa wakati huu ambao kunaonekana kuwepo kwa msuguano mkubwa kati ya nahodha huyo na baadhi ya mabosi zake.

Messi, ambaye hajasaini mkataba mpya huku huu wa sasa ukifikia tamati mwaka 2021, anaweza kuondoka muda wowote kutokana na kuwepo kwa kipengele ki-nachomruhusu kuondoka bure kila mwishoni mwa msimu kama akitaka.

Kipengele hicho kimekuwa mwiba mchungu kwa mabosi na mashabiki wa Barcelona kila inapofika mwishoni mwa msimu, ambapo Bartomeu kasisitiza kuwa Messi anabaki kuwa mali yao. “Jamani tulieni na ondoeni shaka kabisa, Messi amenihakikishia kuwa ataendelea kuwa nasi hadi hapo atakapomaliza soka lake na kustaafu rasmi.

Hapa ndio sehemu ambayo Messi anafura-hia kuwepo na kuinjoyi maisha ya soka,” alisema bosi huyo. Mbali na Inter Milan, klabu nyingine za Man City, PSG na Juventus nazo zinatajwa kuvutiwa na mpango wa kumnasa Messi.