Marefa wa 4-1 wapewa shoo ya Simba

Muktasari:

MAREFA watatu kati ya sita waliochezesha mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga, wamepangwa kuchezesha mechi ya fainali ya mashindano hayo kati ya Simba na Namungo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

MAREFA watatu kati ya sita waliochezesha mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga, wamepangwa kuchezesha mechi ya fainali ya mashindano hayo kati ya Simba na Namungo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

Waamuzi hao ni Abubakar Mturo kutoka Mtwara, Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam na Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jana, imeeleza kuwa mchezo huo wa fainali ambao utachezwa Jumapili, Agosti 2 kuanzia saa 9.00 Alasiri utachezeshwa na waamuzi sita.

Abubakar Mturo ambaye katika mechi ya nusu fainali baina ya Yanga na Simba alikuwa ni mwamuzi wa akiba ndiye atakayesimama katikati kuchezesha mchezo wa fainali akisaidiwa na refa msaidizi Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ambaye naye alichezesha mechi iliyopita ya watani wa jadi ya mashindano hayo msimu huu.

Aidha, mwamuzi Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam ambaye ndiye aliyekuwa refa wa kati katika mchezo wa nusu fainali ambao Simba iliichapa Yanga mabao 4-1 wiki tatu zilizopita, safari hii ndiye atakuwa refa wa akiba katika mchezo wa fainali.

Ukiondoa waamuzi hao watatu, kutakuwa na marefa wengine wawili ambao watasimama nyuma ya goli la kila timu ambapo upande mmoja atakuwapo refa msaidizi, Abdulaziz Ally kutoka Arusha huku kwingine akipangwa Hamdan Said wa Mtwara.

Kamishna wa mchezo atakuwa ni Omary Gindi wa Kigoma, Mtathmini wa waamuzi amepangwa kuwa Soud Abdi wakati mkufunzi wa waamuzi akiwa ni Israel Mjuni.

Refa Abubakar Mturo atakayechezesha mechi hiyo ya fainali, anakumbukwa kwa makosa aliyowahi kuyafanya katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya Yanga na Lipuli uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Februari 05, 2020 ambao Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kosa mojawapo lilikuwa ni kuamua pigo la kona kuelekezwa langoni mwa Yanga, baada ya kipa Metacha Mnata kuurudisha uwanjani mpira ambao tayari ulikuwa umeshaingia langoni akiwa ameushikilia kwenye nguzo ya lango lao.

Refa Mturo alifungiwa miezi mitatu kwa kosa hilo, adhabu ambayo ameshaitumikia.

 

KOCHA NAMUNGO

Kocha Mkuu wa Namungo, Hitimana Thiery amesisitiza kwamba wako tayari kwa mchezo huo na akili yao iko uwanjani. Alisema Simba iko bora zaidi kwa kila mchezaji na hata kitimu tofauti na kikosi chake, hivyo mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa zaidi ingawa wanakwenda kucheza soka lao na wana uhakika wa ushindi.

“Simba kwanza tunatakiwa kuipa heshima yake, imetwaa ubingwa wa ligi na sasa iko fainali ya FA inaonyesha kwa jinsi gani iko bora, lakini mipango ya Mungu ndiyo itaamua nani atoke na matokeo katika mchezo huo.”

Hitimana aliwataja baadhi ya wachezaji wanaompa hofu kwenye fainali hiyo kuwa ni Clatous Chama, Luiz Miquissone, Francis Kahata na John Bocco huku akisisitiza kikosi hicho kinapata matokeo kutokana na timu hiyo kucheza kitimu zaidi ya uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.

 

KOCHA SIMBA

Simba ilipiga tizi la mwisho jana asubuhi jijini Mbeya na mchana ilisafiri kwenda Sumbawanga tayari kwa mchezo huo.

“Maandalizi ni mazuri kila mmoja yupo sawa. Jambo muhimu ni kujiandaa kiakili kucheza kwenye uwanja wa kawaida na kuwa tayari kushinda mataji mawili kwenye msimu huu,” alisema Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alipoizungumzia fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu hadi kwenye vibandaumiza.