Toto Africans yatua TFF sakata la kushuka Daraja

Muktasari:

Timu hiyo kongwe nchini ambayo iliwahi kushiriki Ligi Kuu na kuzihenyesha Simba na Yanga, ilimaliza Ligi Daraja la Pili kwa kichapo cha mabao 2-0 na kushuka Daraja hadi ngazi ya Mkoa baada ya kuambulia pointi 12 tu.

Uongozi wa Toto Africans umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa haki wakidai kufanyiwa hujuma na wapinzani wao Kasulu Red Stars kwa kuwachezesha ‘mamluki’ katika mechi ya mwisho ya Ligi Daraja la Pili.

Timu hiyo kongwe nchini ambayo iliwahi kushiriki Ligi Kuu na kuzihenyesha Simba na Yanga, ilimaliza Ligi Daraja la Pili kwa kichapo cha mabao 2-0 na kushuka Daraja hadi ngazi ya Mkoa baada ya kuambulia pointi 12 tu.

Mmoja wa viongozi wa Klabu hiyo, Beatus Madenge alisema katika mchezo huo ambao ulipigwa uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, wenyeji Kasulu Red Star waliwachezesha wachezaji ambao hawakustahili.

Alisema kikosi kizima cha wachezaji 11 wote walighushi kadi akibainisha kuwa kadi zilizotumika zilionekana wazi kuwa na mapungufu mengi tofauti na zile zilizotoka Shirikisho.

“Kimsingi tunaiomba Bodi ya Ligi na TFF waingilie kati na kutoa haki, haiwezekani timu inaingiza wachezaji kwa kufoji kadi, Klabu zinatumia gharama kubwa kujiendesha” alisema Mjumbe huyo wa kamati ya utendaji.

Hata hivyo Kiongozi huyo alibainisha kuwa wakati mchezo huo ukiendelea walitoa taarifa kwa mamlaka (TFF), ambapo waliambiwa kuendelea na mechi, lakini wakiandika barua na vielelezo, jambo ambalo walilitekeleza.

 Mwenyekiti wa Klabu ya Kasulu Red Stars, Jafari Idd alisema kawaida ya timu inapopoteza mchezo wake, huibuka na visingizio na kwamba usajili wa wachezaji wao waliufanyia TFF.

“Wapeleke malalamiko yao TFF ambapo ndio tulifanyia usajili, unajua mambo ya mpira timu inapokosa ushindi huibuka na sababu nyingi, lazima wakubali matokeo” alisema