Mkwasa ataka umiliki wa mpira Yanga

Muktasari:

Yanga ilianza mazoezi yake siku ya Jumanne kujiandaa na mechi zilizosalia za Ligi Kuu ambazo zitaanza kuchezwa kuanzia Juni 13

KOCHA msaidizi wa klabu ya Yanga, Charles Mkwasa ameonyesha kwamba hana mambo mengi katika mazoezi ya kikosi chake baada ya kuwataka wachezaji wake kucheza mpira zaidi kuliko kitu chochote.

Mwanaspoti Online ambalo limeshuhudia mazoezi hayo katika uwanja wa chuo cha Sheria,liliona kocha huyo akifanyisha mazoezi ya kuchezea mpira tu.

Mkwasa wakati mazoezi yanaanza hakuwataka wachezaji wake wakimbie badala yake aliwapanga kwa makundi kisha wacheze mpira kwa kupiga danadana (kontroo) na pia kupigana chenga.

Baada ya hapo Mkwasa aliwapa zoezi la kukimbia katika viunzi na zoezi hilo alilisimamia kwa umakini huku wachezaji wakionekana wepesi.

Programu zote zilizokuwa zikitolewa wachezaji walikuwa wakizifanya kwa ufasaha jambo lililooneka kumridhisha Mkwasa.

Walipotoka katika viunzi Mkwasa alipanga koni kwa mtindo wa kugawa pande tatu na kisha kuwapa mazoezi ya kucheza mpira.

Kilichofanyika katika upande mmoja wa goli alimuweka beki Said Makapu na Kelvin Yonda kisha walikuwa wakimkaba Ditram Nchimbi.

Katika upande wa katikati uliotenganishwa na koni, walikuwa wanacheza mabeki na viungo ambao walikuwa wanatakiwa kuhakikisha wanapenyeza mipira kwa Nchimbi ili aweze kufunga.

Upande wa tatu ulikuwa na mabeki Andrew Vicent 'Dante' na Ally Ally ambao walikuwa wakimkaba Tariq Seif.

Viungo waliokuwa wanacheza katikati, wao walikuwa wanashambulia kotekote pindi tu mpira unapoanzishiwa.

Mazoezi ya kuchezea mpira huwa yanamfanya mchezaji kuzidi kujiamini pindi anapokuwa nao mguuni.