Kagere atua na angalizo

Muktasari:

Kagere anaongoza msimamo wa ufungaji bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu akiwa na mabao 19 na aliichukua tuzo hiyo msimu uliopita baada ya kupachika mabao 23

Mshambuliaji nyota wa Simba, Meddie Kagere kutoka Rwanda, amewasili leo jijini Dar es Salaam huku akiwakumbusha wachezaji wenzake kuwa hategemei kuona wakipoteza nafasi ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Kagere aliyekuwa nchini Rwanda, aliwasili leo mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tayari kwa kuungana na wenzake kwa ajili ya kumalizia mechi zilizobaki za Ligi Kuu na Kombe la Azam Sports Federation.
Akizungumza na tovuti ya Simba, www.simbasc.co.tz muda mfupi baada ya kutua, Kagere alisema kuwa uwepo wao kileleni mwa msimamo wa Ligi ni fursa muhimu ambayo hawatakiwi kuipoteza.
"Siamini kwamba kuna mchezaji yeyote ambaye ameshafika juu halafu akakubali kuanguka.Kama uko juu uko juu huwezi kukubali kulipoteza," alisema Kagere.
Hata hivyo Kagere alisema kuwa kutokana na ligi kusimama kwa muda mrefu bila wachezaji kucheza mechi, kuna kazi kubwa inayopaswa kufanyika ili wawe na ubora waliokuwa nao kabla ligi na mashindano mengine hayajasimamishwa na serikali kama miongoni mwa hatua za kukabiliana na virusi vya Corona
"Kilichotokea kwa wachezaji kimetuathiri kwa sababu tumekaa kwa muda mrefu bila kucheza mechi. Kama unataka kuwa uko levo ya juu, jambo la kwanza ni kuwa na ufiti wa mechi.
Ufiti wa mechi ni ishu ya kila mchezaji huwezi kufanya mazoezi kwa miezi miwili lakini ukiukosa kwa kutocheza mechi au za kirafiki sikatai kwamba inaweza kuwa na athari kwa kila mchezaji na inahitajika mechi mbili au tatu urudi katika kiwango chako cha kawaida.
Programu na yale yote tuliyoelekezwa wakati wa mapumziko nimeyafanya kama nilivyohitajika na nimeyatekeleza inavyotakiwa.Nilikuwa nazungumza nao (makocha) wakajua maendeleo yangu," alisema Kagere.
Katika hatua nyingine, Kagere alisema uamuzi wa mechi zilizobakia kuchezwa bila uwepo wa mashabiki viwanjani, utapunguza hamasa kwa wachezaji
"Haiwezi kuwa kama tulivyozoea. Kikubwa kutakuwa na mabadiliko kwa sababu hakutokuwa na watu wakija mazoezini, uwanjani kutokuwa na watu wachache kinyume na vile tulivyozoea kwamba watu wanajaa uwanjani na kutushangilia," alisema Kagere.
Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 71 na inahitaji ushindi katika mechi tano tu kati ya 10 ilizobakiza ili itwae ubingwa ambao utaifanya iwe imechukua taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo.