Eti! Kiungo Bruno anawafundisha soka nyota wa Manchester United

Muktasari:

Kiungo huyo Mreno kwa haraka sana amezoea mazingira ya Old Trafford na kuwa mchezaji nyota ndani ya muda mfupi tu aliotua kwenye kikosi hicho.

MANCHESTER, ENGLAND. Nyota wa Watford, Troy Deeney amesema kitu ambacho kiungo Bruno Fernandes anachokifanya tangu atue Manchester United ni kuwafundisha mpira mastaa wa timu hiyo.

Kiungo huyo Mreno kwa haraka sana amezoea mazingira ya Old Trafford na kuwa mchezaji nyota ndani ya muda mfupi tu aliotua kwenye kikosi hicho.
Wengi wanaamini kwenye kiwango bora cha Fernandes, ambaye tayari ameshabeba tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Februari, huku akimaliza kabisa ule wasiwasi uliokuwa ukiwasumbua mashabiki wa Man United juu ya maisha yatakavyokuwa Paul Pogb akiondoka mwisho wa msimu.
Lakini, sasa hofu hiyo haipo tena na kiungo huyo wa Kireno analinganishwa na Paul Scholes kutokana na mavitu yake ya uwanjani. Staa wa Watford, Deeney alisema ubora wa Fernandes unamfanya hata Pogba kuanza kujifikiria upya kuhusu hatima yake, abaki aondoke.
"Kama ataondoka, hiyo wala haitakuwa tatizo tena," alisema.
"Nilimsikia uwanjani, wakati mwingine alikuwa akiwafundisha mpir wenzake. Utashangaa, lakini sisi wachezaji licha ya kwamba tumekuwa tukifanya mazozi, kipindi kingine unahitaji mtu wa kukupandisha kiwango chako. Bruno anafanya hicho kitu."
Man United walikuwa kwenye ubora wao wakati Ligi Kuu England inasimamishwa kutokana na janga la virusi vya corona.