Simba wamponza straika wa Stand United

MSHAMBULIAJI wa Stand United, Miraji Salehe amesema tangu afunge bao katika mchezo na Simba amekuwa na wakati mgumu kwenye Ligi Daraja la Kwanza kwani amekuwa akikamiwa kinoma na mabeki wa timu pinzani.
Salehe aling’ara katika mchezo huo wa kombe la FA ambapo alifunga bao la kusawazisha la 1-1  katika pambano la kusaka tiketi ya kucheza robo fainali ambapo Simba walishinda kwa mikwaju ya penalti ya 3-2 kwenye mtanange uliopigwa mjini Shinyanga.
Amesema kabla ya kucheza na Simba alikuwa hapati tabu kwenye mechi zao lakini baada ya kufunga bao katika mchezo wao wa kombe la FA mambo yalianza kubadilika kwani amekuwa akikutana na upinzani mkali kutoka kwa mabeki hao.
Salehe alisema tayari amecheza mechi tatu baada ya kutolewa na Simba lakini katika michezo hiyo amefunga bao moja pekee tena kwa mbinde tofauti na mwanzo kabla ya kutopata upinzani mkubwa.

“Tumecheza na Geita Gold, Gipco na Mashujaa baada ya kucheza na Simba lakini hizi mechi nimekutana na upinzani mkubwa sana angalia nimefunga bao moja tu ambalo nalo nilipambana sana,” alisema Salehe.

Kwa sasa amefunga mabao nane ambapo katika kipindi hiki atajifua ili atakaporejea kwenye timu awe fiti kupambana na mabeki hao ambao kwa sasa wamekuwa wakimchezea undava.