Chobanka hesabu zote Ubingwa TWPL

KOCHA Mkuu wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka

KOCHA Mkuu wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka amesema licha ya Ligi kusimama wakiwa nafasi ya tatu, lakini matumaini yao msimu huu ni kubeba ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chake.
Kwa sasa Ligi Kuu ya Wanawake na michezo mingine imesimama kwa muda, ambapo Alliance Girls wapo nafasi ya tatu wakati na pointi 28 ikishuka uwanjani mara 11, huku JKT Queens wakiongoza alama 29 baada ya mechi 13.
Chobanka alisema msimu huu anaona dalili za kubeba taji na kwamba ishu ya kuwa nafasi ya tatu kwa sasa haiwezi kumpa presha kwani ana faida ya michezo miwili dhidi ya waliopo juu yake.
Alisema mkakati wake ni kuhakikisha timu itakaporudi kambini  mapema Aprili, atawaandaa vyema wachezaji wake ili kurudisha kasi waliyokuwa nayo na kuweza kufikia malengo yao.
“Msimu huu tumejipanga kwa ubingwa, tunahitaji kushinda mechi zetu za viporo kisha kuanza kusaka ushindi kwenye michezo iliyobaki, ninajivunia kikosi changu” alisema Chobanka.
Kocha huyo alisema ishu ya Corona imewatibulia mambo kutokana na kwamba mipango yao imesimama na kwamba inaweza kuathiri program za kiufundi.
“Kusimama kwa ratiba ya mashindano inaathiri hasa programu kwa sababu itatupasa benchi la ufundi kuanza upya pale tutakaporudi kambini, lakini ushindani ni mkali na tumedhamiria kufanya vizuri” alisema Kocha huyo.