Diamond Platnumz afikisha watazamaji 900 milioni youtube

Monday March 23 2020

Mwanaspoti, Tanzania, Diamond Platnumz afikisha, watazamaji 900 milioni youtube, wimbo Yope

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Mwanamuziki Diamond Platnumz amefikisha watu 903milioni waliotazama kazi zake mbalimbali katika mtandao wa Youtube hadi leo Jumatatu Machi 23, 2020 saa 7 mchana.

Diamond jina lake halisi ni Nassib Abdul alijiunga na mtandao huo Juni 12, 2011 na amepata watazamaji wengi kutokana na kazi zake mbalimbali anazoziweka katika mtandao huo.

Diamond katika akaunti yake ya Youtube tayari ana wafusi 3.28 milioni akiwa msanii wa kwanza Tanzania kuwa na wafuasi wengi katika mtandao huo.

Baadhi ya matukio anayoyaweka katika mtandao huo ni shoo anazozifanya ndani na nje ya nchi, matangazo ya bidhaa na huduma, matukio ya kijamii anayoshiriki na utayarishaji wa video za nyimbo zake.

Mbali na hilo pia amekuwa akiweka picha mnato anazopiga akiwa peke yake au na watu wake wa karibu, wakiwemo baadhi ya mashabiki zake wanaocheza nyimbo zake mbalimbali.

Mathalani wimbo Yope aliyoshirikishwa na msanii Innos’ B wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umetazamwa mara 73milioni ndani ya miezi sita, kuwa wimbo unaoongoza kwa kutazamwa zaidi.

Advertisement

Kutokana na idadi hiyo ya watazamaji, Diamond amewaacha mbali wasanii wa Afrika wanaofanya vizuri katika tasnia ya muziki akiwemo msanii Wizkid mwenye watazamaji 792milioni.

Davido ana watazamaji 543milioni na Burnaboy ana watazamaji 429milioni.

Tangu alipoanza muziki miaka 10 iliyopita, Diamond ameshaachia nyimbo mbalimbali ikiwemo Mdogo mdogo, Nitampata wapi ,Inama aliomshirikisha Fally Ipupa, Number One Remix aliomshirikisha Davido, Baba Lao, I Miss You  na The One.

Advertisement