TFF: Kagere, Morrison, Miquissone msirudi Tanzania

Muktasari:

Karia amesema wao kama TFF hawajatoa likizo kwa wachezaji bali Serikali imesimamisha michezo kwa lengo la kupambana na janga la Corona hivyo klabu zisitumie mapumziko ya siku 30 za ligi kama likizo.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),Wallace Karia ameziambia klabu za Ligi Kuu Bara endapo zitawaruhusu wachezaji wao wa kigeni kurejea katika nchi zao basi hawatawaruhusu tena kurejea na kushiriki Ligi Kuu hapa nchini kwa sasa.
Karia amesema wao kama TFF hawajatoa likizo kwa wachezaji bali Serikali imesimamisha michezo kwa lengo la kupambana na janga la Corona hivyo klabu zisitumie mapumziko ya siku 30 za ligi kama likizo.
“Tunazikumbusha klabu na viongozi  wake kuwa  hatukutoa likizo kwani nimeshapata taarifa kuwa kuna baadhi ya klabu ambazo zina wachezaji wa kigeni au wafanyakazi wa kigeni wanafanya matayarisho ya kuwaruhusu kwenda kwenye nchi zao sasa  hiyo itakuwa ni kinyume na maelekezo ya serikali
  “Kwa sababu  watakapoenda nje sisi tutawasiliana na vyombo vya serikali na hatutawaruhusu tena kurudi hapa nchini hata kama muda wa siku 30 wa kusimama kwa ligi utakuwa umepita kwani tukiwaruhusu kuingia hata kama wakati mda umepita  itakuwa tunafanya mchezo .
“Si ajabu tayari kutakuwa na hali ya unafuu lakini wao wametoka huko hatujui wametoka wapi ila hatuwawaruhusu kushiriki kwenye michezo yetu na tutawasiliana na vyombo vya Serikali kuhakikisha hatuwaruhusu kurudi tena nchini kwa kipindi hiki ambacho tutakuwa kwenye tahadhari.
“Sio huu mwezi mmoja tu  ambao tunatakiwa kukaa katika tahadhari ila ni mwezi wa kuhakikisha maambukizi yasiendelee na hali ikiwa nzuri tunaweza kuendelea na shughuli zetu za kawaida sasa tukiendelea na shughuli zetu halafu tulishawaruhusu watu wakaendea kwenye nchi zao na hatujui tahadhari ambazo nchi hizo zilichukua, zimeathirika vipi hivyo tukithubutu kuwaruhusu tu tutakuwa kama tunafanya mchezo “alisema Karia.
Tayari staa wa Simba, Meddie Kagere ameshakwenda kwao kupumzika huku Bernard Morrison wa Yanga na Luis Jose wa Simba wakisikilizia uwezekano wa kuchomoka fasta.
Naye Ofisa Habari wa Uhamiaji, Ally Mtanda  amesema kwa upande wao wameongeza muda wa vibali vya wachezaji na makocha wa kigeni kutokana na janga hili la Corona.
“Idara ya uhamiaji imewaongezea muda wachezaji na makocha wa kigeni waliopo hapa nchini na  sio wao tu bali wageni wote walioingia hapa nchini ambao muda wao  wa kukaa hapa umeisha na hawawezi kurejea katika mataifa yao kutokana na  Corona,” alisema Mtanda.