Simu moja tu ya kocha ilivyomnasa Michael Lema

Muktasari:

Baada ya kutoka jeshini ambako alienda kupata mafunzo ya ukakamavu kwa mujibu wa katiba yao, Lema hakuona sababu ya kuendelea kusota benchi Sturm Graz

SIMU ya Markus Schopp kocha wa TSV Hartberg, ilitosha kumshawishi nyota wa Kitanzania, Michael Lema kufanya maamuzi ya kujiunga na klabu hiyo kwa mkopo akitokea Sturm Graz inayoshiriki Ligi Kuu Austria.
Baada ya kutoka jeshini ambako alienda kupata mafunzo ya ukakamavu kwa mujibu wa katiba yao, Lema hakuona sababu ya kuendelea kusota benchi  wakati huo akiwa ameombwa kuungana na Schopp huko Styria yaliyopo maskani ya timu hiyo.
Akielezea mchakato ulivyokuwa Lema, alisema Schopp alimpigia simu na kutaka wafanye kazi pamoja hakuwa na muda wa kuwaza maisha nje ya klabu yake iliyomlea tangu akiwa mtoto, alifanya maamuzi huku akiwashirikisha wasimamizi wake.
“Nitakuwa hapa hadi mwishoni mwa msimu, nimepata pahala pengine ambako ni nyumbani, wamenipokea vizuri na ninaimani kuwa tutashirikiana vizuri kuhakikisha tunakuwa na msimu mzuri,” alisema kinda huyo.
Lema amepanga kutumia fursa ya kuichezea kwa mkopo TSV Hartberg ambayo inashiriki Ligi Kuu Austria kama sehemu ya kujiweka sokoni ili majira ya kiangazi atimke nchini humo ambako alikulia.
“Natamani kucheza Ligi ya Ujeruman, sitamani iishie kuwa ndoto. Ni moja ya ligi kubwa Ulaya ambayo wengi wamekuwa wakiifuatilia tofauti na hapa nilipo,” alisema.