Simba yatakata Kirumba, Minziro afunguka

Muktasari:

Huu ni mwendeleza wa Simba kuinea Alliance ambayo tangu imepanda daraja haijawahi kushinda wala kupata sare mbele ya Simba.

MABAO manne ya Simba yaliyofungwa na  Jonas Mkude, Medie Kagere, Cletous Chama na Hassan Dilunga yameipa ushindi mnono timu yao kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza walipocheza na Alliance FC, jioni ya leo huku wakiendelea kujiimarisha kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mabingwa hao watetezi Simba imeiduwaza Alliance inayonolewa na beki wa zamani wa Yanga, Fred Felix Minziro  kwa kipigo cha mabao 4-1, wakitokea nyuma kwa bao moja na kocha huyo mzawa akipewa kadi ya njano na mwamuzi wa mchezo huo.

Alliance walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa beki wa kuliaIsrael Patrick 'Mwenda' kwa shuti kali la mpira wa adhabu ndogo lililomshinda kipa Benno Kakolanya na lililokwenda moja kwa moja na kujaa wavuni.

Wakiamini wanakwenda mapumziko wakiwa wanaongoza, kiungo Jonas Mkude aliwaduwaza Alliance kwa bao safi la shuti nje kidogo ya 18, dakika tatu za nyongeza kipindi cha kwanza na timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili, Simba ilirudi kwa kasi na kupachika mabao dakika ya 58, 63 na 72 huku kocha Fred Felix Minziro akionywa na mwamuzi kwa kupewa kadi ya njano baada ya kuonekana kuzoza wakati Simba ikielekea kupiga faulo langoni mwa timu yake iliyozaa bao la pili lililofungwa na Kagere kwa kichwa ambaye alifikisha bao lake la 11 msimu huu.

Dakika tano baada ya bao hilo, Chama aliandika bao la tatu kwa faulo iliyokwenda moja kwa moja langoni mwa Alliance katika maeneo yale yale ambayo Alliance walipata bao la kuongoza kwa faulo,

Dilunga aliitimisha kalamu ya mabao baada ya kuifungia Simba bao la nne akipokea pasi safi kutoka kwa kiungo mbunifu Sharaf Eldin Shiboub.

Kwa ushindi huo wa mabao 4-1, Simba imeendelea kujiimarisha kileleni katika msimamo wa ligi ikiongoza kwa kufikisha pointi 41 katika mechi 16.

Kocha wa Alliance, Minziro mara baada ya mechi kumalizika alisema malengo yao yalishindwa kukamilika haswa katika kipindi cha pili baada ya wachezaji wake kukubali kufungwa mabao matatu ambayo yalitokana na kukosa umakini kwenye kukaba.

Akizungumzia mchezo huo, kocha Minziro alisema licha ya wao kuanza vizuri kwa kuongoza lakini walishindwa kuendelea na kiwango hicho kipindi cha pili kwani muda ulivyokuwa unazidi kwenda chini walipoteza ubora ambao walianza nao.

"Malengo yetu yalivurugika, hatukuwa vizuri katika umakini, hivyo hatuna budi kujipanga upya katika mechi zinazokuja ili timu yetu iweze kufanya vizuri kwa maana huu ndio mchezo wangu wa kwanza nikiwa kama kocha mkuu," alisema Minziro ambaye kabla ya kutua katika kikosi hiko alikuwa timu ya Pamba ambayo ipo Ligi Daraja La Kwanza.