Sven aivunja pacha ya Kagere, Bocco kimtindo Simba

Muktasari:

Kagere aliibuka kinara wa mabao akifunga 23 huku Bocco akifunga 14 wakichangia kwenye idadi ya jumla ya mabao 77 ambayo walifunga Simba msimu mzima.

KOCHA wa Simba, Mbelgiji Sven Vandebroeck, amesema anaamini mfumo wa kutumia mshambuliaji mmoja asilia ndio unampa matokeo mazuri na kwamba, ndio ataendelea kuutumia.
Kwa muda mrefu Simba imekuwa ikitumia mfumo wa washambuliaji wawili ikiwatumia zaidi Meddie Kagere na John Bocco na kuwapa matokeo mazuri yenye mabao mengi, lakini tangu ametua na kuiongoza Simba kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara, Sven amekuwa akitumia mshambuliaji mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti jana, Sven alisema katika mechi zijazo ataendelea kutumia mshambuliaji mmoja kwa kuwa, ndio falsafa yake kwenye soka.
Hata hivyo, alisema kuwa kila kocha amekuwa na mbinu zake anazoziamini katika kumpatia matokeo bora uwanjani na kuipa timu yake mafanikio.
“Mshambuliaji mmoja asilia ndio falsafa yangu ambayo inanipa matokeo, lakini nyuma yake kunaweza kuwa na kiungo wa pembeni kama alivyo Francis Kahata, Sharaf Shiboub au Clatous Chama. 
“Sishangazwi kuwa Kagere na Bocco msimu uliopita walifunga mabao mengi, bali naamini nitatumia mmoja na mwingine atakuwa mbadala kulingana na mechi ilivyo, lakini nitatoa muda wa kupokezana.
“Lakini, bado tunaweza kuwatumia wote katika baadhi ya mechi kama tutakuwa na malengo fulani ila viungo wa asili lazima wawepo kufanya kazi yao kikamilifu,” alisema.
Rekodi zinaonesha msimu uliopita Bocco na Kagere walimaliza Ligi Kuu Bara wakifunga mabao 37 kwenye mechi ambazo walicheza pamoja.
Katika msimu huo, Kagere aliibuka kinara wa mabao akifunga 23 huku Bocco akifunga 14 wakichangia kwenye idadi ya jumla ya mabao 77 ambayo walifunga Simba msimu mzima.