Polisi wamuokoa mwamuzi Coastal Union ikilazimishwa sare, Mbeya City, Singida United zaua

Saturday January 11 2020

Mwanaspoti-Polisi-mwamuzi-Coastal Union-Mbeya City-JKT Tanzania zaua

 

By Thomas Ng’itu, Burhan Yakubu

Dar es Salaam. Polisi walilazimika kutumia nguvu kuokoa maisha ya mwamuzi Listoni Liyali baada ya wenyeji Coastal Union kulazimishwa sare 1-1 na Biashara United kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mashabiki wa Coastal Union baada ya filimbi ya mwisho walivamia uwanja wakitaka kumpiga mwamuzi Liyali kutoka Dar es Salaam wakimshutumu kwa kuchezesha vibaya mechi hiyo ndipo polisi walipoingia uwanjani na kumtoa mwamuzi huyo.

Wenyeji Coastal Union walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika 47, kupitia kwa Ayoub Lyanga, kabla ya Biashara United kusawazisha katika dakika 90, kupitia Kelvin Friday.

Mbeya City imefufuka kwa kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Bao la Kelvin Kayongo alilofunga dakika 70 liliwafanya Mbeya City kubaki katika nafasi  18  wakiwa na pointi 13 na kuwaacha Ndanda wakiendelea kusalia katika nafasi ya 19 wakiwa na pointi tisa.

Mchezo huu ulikuwa ni vita kwa timu hizi ambazo zipo mkiani zikiwa katika harakati ya kujikwamua na janga la kushuka daraja.

Advertisement

Katika michezo mingine Singida United imepata ushindi bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting shukrani kwa goli la Elinywesia Sumbi alilofunga dakika 68 na kupanda nafasi moja kutoka mkiani.

Mabao mawili ya Sixtus Sabilo yametosha kuipa Polisi Tanzania ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar huku bao la kufutia machozi kwa Kagera Sugar likifungwa na Kelvin Sabato.

Ushindi huo unawafanya Polisi kupanda hadi nafasi ya 8 kutoka 11 wakiwa na pointi 24.

Mbao Fc watajilaumu wenyewe kwa kukosa ushindi licha ya kuongoza kwa mabao 2-1 dhidi JKT Tanzania hadi dakika 90, kabla ya Mgandila Shaban kuwasazishia maafande hao na kufanya mechi kumalizika kwa matokeo kuwa 2-2.

Katika mchezo huo mabao ya Mbao yalifungwa na Kauswa Manumbu na Waziri Junior, huku yale ya JKT Tanzania yakifungwa na Daniel Lyanga na Mgandila Shabani.

JKT Tanzania imepanda kutoka nafasi ya saba hadi ya nne ikiwa na pointi 26 huku Mbao wakipanda nafasi moja wakitoka nafasi 15 kwenda 14 wakiwa na pointi 18.

Advertisement