Mariga sasa aipimia weather kiti cha Mwendwa, FKF

Muktasari:

Duru zinaarifu kuwa Mariga kwa sasa anaipimia weather kiti hicho cha Mwendwa na ni kwamba  tayari kaanza kujipanga kujitosa kwenye mbio hizo za kumng’oa rais wa sasa, Nick Mwendwa madarakani.

HUKU Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) likiwa limeamrisha FKF kuhakikisha inaandaa uchaguzi wake mkuu kufikia Machi, mwaka huu baada ya uchaguzi wa Disemba 7 kufutiliwa mbali, kuna uwezekano kiungo McDonald Mariga naye akajiongeza kwenye hesabu za kusaka urais wa chombo hicho.
Duru zinaarifu kuwa Mariga kwa sasa anaipimia weather kiti hicho cha Mwendwa na ni kwamba  tayari kaanza kujipanga kujitosa kwenye mbio hizo za kumng’oa rais wa sasa, Nick Mwendwa madarakani.
Hili linajiri baada yake kustaafu soka ghafla na kisha kujitosa kwenye siasa ambapo aligombea kiti cha ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra na kuishia kumaliza wa pili.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza, sapoti hiyo aliyoipata anasemekana kaiona kuwa kubwa sana hivyo kumfanya kuamini kwamba kama akigombea urais wa FKF basi atapita nalo.
Mariga ana fursa hiyo baada ya  FKF kuamuriwa na mahakama ya kimichezo nchini kurudia uchaguzi huo kwa kuhakikisha inabuni bodi mpya ya kusimamia uchaguzi.|
Pili ilitakiwa kuwaruhusu baadhi ya wadau wakiwemo shirikisho la makocha na marefa waliokuwa wamefungiwa nje kutoshiriki uchaguzi huo.
Sasa basi ikiwa Mariga atajiongeza rasmi basi, atakumbuna na upinzani kutoka kwa Sam Nyamwenya anayeendesha kampeni zake kwa fujo sana, Gavana wa zamani wa Vihiga Moses Akaranga, mwenyekiti wa zamani wa AFC Leopards Alex Ole Magelo pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Lodrvick Aduda.