VIDEO: Yanga, Zahera wanachaguo moja tu kwa Pyramids leo

Muktasari:

Presha kubwa katika yote yatakayojadiliwa ni juu ya hatma ya Zahera kwani kuna vigogo wengi wanaonekana kutokukubaliana na uwezo wake.

Dar es Salaam. Yanga inatakiwa kufanya jambo moja tu leo ushindi mbele ya wenyeji wao Pyramids katika mchezo wa Kombe La Shirikisho Afrika utakaopigwa Saa 3:00 usiku.

Matokeo ya huko yanaweza kutibua hali mbaya au kuituliza klabu hapa nyumbani na kubwa ni juu ya hatma ya kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera.
Yanga ambayo ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji wao katika mchezo wa kwanza hapa nyumbani, salama yao ni moja tu kushinda kwa mabao 2-0 kisha watinge hatua ya makundi ingawa mlima huo unaonekana mrefu kwa kikosi hicho.
Baada ya kutua nchini humo kuanzia alfajiri ya alhamisi  Oktoba 31, Yanga ilifanya mazoezi ya kwanza siku hiyo na jana usiku walitarajia kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa June 30, ambao utatumika kwa mchezo huo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela ameliambia gazeti hili, tangu wafike morali ya vijana wao iko juu kuelekea mchezo huo.
“Mpaka sasa (jana) tuko sawa, kila kitu kipo vizuri, vijana wanaonekana wamechangamka, morali yao iko juu na matumaini  ni makubwa, muhimu ni kuomba vijana waamke vizuri,” alisema Mwakalebela.
“Hoteli tunayotumia ni nzuri na tuko vizuri na tunapambana kiukweli kuweka mambo sawa kuelekea mchezo huo.”

Msikie Zahera
Wakati bosi wa klabu akiyasema hayo, kocha wao Zahera alisema jana anachoomba ni utulivu katika mchezo huo kwani wanatambua ubora wa wapinzani wao.
Zahera alisema wanatambua wanakutana na Pyramids yenye nguvu kubwa ya fedha lakini akili yao ni kutafuta ushindi.
“Tumekuja na wachezaji wote ambao wako sawa kiafya, hatuwezi kuogopa lakini tuna jukumu la kupambana kupata matokeo.
“Tutamkosa Kelvin (Yondani sawa, lakini nafurahi tutakuwa na Lamine (Moro) hakuna shida tutakuwa na mabadiliko kidogo kulingana na mazoezi ya baadaye usiku (jana).

Bosi Pyramids  atimuliwa hotelini
Wakati Zahera akiyasema hayo kigogo mmoja wa Pyramids ametimuliwa katika hoteli ya Yanga baada ya kufanikiwa kupenya na kuingia ndani ya hoteli hiyo.
Kigogo huyo inaelezwa alifanikiwa kuingia hotelini humo kisha kufanikiwa kukutana na mshambuliaji Sadney Urikhob na hapo ndipo alipokutwa na Mkuu wa Msafara kutoka TFF, Novatus Lufano kisha kunusurika kipigo kisha kutimuliwa.
Zahera amethibitisha hilo akisema baada ya kigogo kutimuliwa wakifanya mazungumzo na Sadney kujua alichohitaji.
“Hawa watu wana pesa sana nawaogopa sana, ni kweli tulimkuta huyo kiongozi wa Pyramids hatujajua alifanikiwa vipi kuingia ndani ya hoteli,” alisema Zahera.
“Tumemuuliza Sadney akasema alikuwa amemsimamisha na kumwomba namba ya simu tu na ndio tulichokuta wanakaribia kupeana namba.”
“Tunalazimika kuwa makini sana huku, hawa jamaa wanajulikana kwa mambo ya ovyo na hata Al Ahly wanajua mambo yao.”

Bongo vigogo  wamkomalia
Wakati Yanga ikipambana hivyo nchini, Misri huku nyuma nyumbani kulikuwa na kikao kizito cha kamati ya utendaji kikifanyika.
Presha kubwa katika yote yatakayojadiliwa ni juu ya hatma ya Zahera kwani kuna vigogo wengi wanaonekana kutokukubaliana na uwezo wake.
Presha inaweza kuongezeka endapo tu kikosi hicho kitapoteza vibaya katika mchezo huo.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini ndani ya vigogo hao pia wapo baadhi wakiwa tofauti na maoni ya wenzao hali ambayo inaweza kuilazimisha kikao hicho kupiga kura kuamua.
Ndani ya saa 48 huenda hatma ya Zahera ikajulikana juu ya nafasi yake ingawa mwenyewe aliliambia Mwanaspoti mapema wala hana hofu na kupoteza kazi hiyo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema jana kama uongozi wamemaliza kila kitu kwa mchezo dhidi ya Pyramids FC wanachosubiri ni utekelezaji wa wachezaji.
Dk Msolla alisema; “Tumeshazungumza na wachezaji pamoja na viongozi waliotangulia Misri wametuhakikishia ushindi ikiwa ni sambamba na kutuambia wachezaji wote waliosafiri wapo salama na wana ari ya ushindani.” Kuhusu kinachozungumzwa kwa sasa kuhusu timu yake na Kocha Zahera alisema ni kutaka kukatishana tamaa tu.
“Mengi yamezungumzwa kuelekea mchezo huo yakiwa ni kukatishana tamaa, wengine wakidai wachezaji wetu hawawezi kupata matokeo ugenini, hilo halijatutoa mchezoni tuna imani nao na lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90.”
Katika mchezo wa leo Yanga inatarajiwa kukichezesha sehemu kubwa ya kikosi kilichoivaa Pyramids jijini Mwanza isipokuwa nafasi za Kelvin Yondani ambaye anatumikia kadi nyekundu akipokewa na Lamine Moro aliyekuwa na adhabu ya kadi kama hiyo katika mechi za awali.
Pia huenda Juma Balinya na Patrick Sibomana wakaanza mchezo huo, huku Issa Bigirimana na Rafael Daud wakitarajiwa nao kuwepo kwenye mchezo huo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.

REKODI ZAITIBULIA
Licha ya matumaini makubwa waliyonayo Yanga, lakini rekodi za Pyramids ikiwa nyumbani na zile za Yanga wanapocheza ugenini na hasa Cairo dhidi ya timu za Misri zinawakataa kabisa.
Sio kucheza Misri, lakini Yanga haina bahati ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao zote za kimataifa walizowahi kuzicheza kwenye nchi za Ukanda wa Afrika Kaskazini ikiwamo Sudan, Libya, Morocco na hata Algeria.
Mara zote Yanga imekuwa ikikumbana na aibu ya kupigwa nyingi, ukiondoa mara moja ilipopata sare ya 1-1 mwaka 1992 dhidi ya Ismailia katika Ligi ya Mabingwa Afrika (enzi za Klabu Bingwa).
Kwa mujibu wa rekodi ambazo zipo ni kwamba nchini Misri pekee, Yanga imeshacheza mara nane dhidi ya timu tatu za Al Ahly, Zamalek na Ismailia na mara zote imepasuka isipokuwa sare moja pekee iliyopata ambayo hata hivyo haikuisaidia kwani ilishjapoteza nyumbani 2-0 na kung’oka.
Mara ya kwanza kwa Yanga ambayo ndio klabu ya kwanza Tanzania kushiriki michuano ya CAf ikifanya hivyo mwaka 1969 na kuishia robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika hatua waliyofikia tena 1970 kwa kung’olewa na Asante Kotoko mara zote, ilianza kucheza na Wamisri mwaka 1982.
Yanga ilienda kuvaana na Al Ahly katika Klabu Bingwa na kubugizwa mabao 5-0 kabla ya kurudi tena mwaka 1988 na kucharazwa 4-0 na hao hao Al Ahly ndipo 1992 ikatoka sare ya Ismailia kwa bao la shuti kali la mbali na aliyekuwa nahodha wao, Kenneth Mkapa.
Mwaka 2009 iliwafuata tena Al Ahly na kucharazwa mabao 3-0 kisha kukukutana na Zamalek mwaka 2012 katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kulala bao 1-0 na kukutana tena na Al Ahly mwaka 2014 na kuchapwa ba0 1-0 na kung’olewa kwa mikwaju ya penalti.
Yanga iliendelea kuwa wateja wa kudumu wa Al Ahly kwani mwaka 2016 ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 na kung’olewa Ligi ya Mabingwa na kufuzu makundi ya Shirikisho msimu huo, lakini mwaka 2000 katika Kombe la Washindi Afrika enzi hizo (sasa Kombe la Shirikisho lililounganishwa na Kombe la CAF) walikumbana na kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Zamalek.
Aidha katika mechi mbili zilizopita za nyumbani za Pyramids haijawahi kupoteza katika Kombe la Shirikisho kwani, iliwachakaza Etoile du Congo ya Congo Brazzaville kwa mabao 4-1 na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya majirani zao wa CR Belouizdad, kazi inayowafanya Yanga kuwa na kibarua kigumu.