Kilichotokea kwa masupastaa wote Wenger aliowataka, akawakosa Asernal

Muktasari:

Nilizungumza na Barcelona, Real Madrid na Inter pia, lakini mechi ya kirafiki dhidi ya Man United, ambayo ilivutiwa na mimi, ilifanya haraka ikanisajili.”

LONDON,ENGLAND. ARSENE Wenger mara zote amekuwa mkweli juu ya kufichua dili zake za usajili alizokuwa akifanya kwenye kikosi cha Arsenal alichodumu nacho kwa zaidi ya miaka 22 kabla ya kuachia ngazi Juni 2018.

Kwenye kikosi hicho cha Arsenal kwa muda wote huo wa miaka 22, Kocha Wenger aliwasajili wachezaji 126 tofauti, lakini kuna wakali wengine, amekiri kuwakosa licha ya kwamba alihitaji kunasa huduma zao. Hii hapa orodha ya masupastaa wa nguvu, ambao Wenger alishindwa kidogo sana kuzinasa saini zao wakakipige Arsenal.

“Unajikuta unaishi kwa kujutia mambo ambayo hukuweza kuyakamilisha,” alisema Wenger akizungumzia wachezaji ambao aliwataka wakakipige Arsenal, lakini imeshindikana kutokea hilo.

1) Cristiano Ronaldo

“Mchezaji anayekuja moja kwa moja akilini ni Ronaldo,” alisema Wenger alipoulizwa wachezaji ambao alikaribia kusajili huko Arsenal. Bila shaka mashabiki wa Arsenal hawatamwelewa kabisa Wenger kwa namna alivyowakosesha huduma ya mchezaji huyo ambaye baadaye alikwenda kushinda tuzo tano za Balon d’Or akitamba na timu nyingine na wao wakiteseka. Ronaldo aliwatesa Arsenal alipokuwa Manchester United.

“Alikuja hapa na mama yake na tulikuwa watu wa karibu sana,” alisema Wenger akimzungumzia Ronaldo.

“Lakini Man United wakaingia na walikuwa na Carlos Queiroz wakati ule, ambaye alikuwa kocha wao. United walicheza na Sporting Lisbon na Ronaldo aliwasumbua sana kwenye mechi, wakamsajili.”

“Unaweza kuona tu, ingekuwaje unakuwa na timu yenye Thierry Henry na Ronaldo pamoja...\Nadhani hilo lingebadili historia ya Arsenal. Sisi tulikuwa na Pauni 4.5 milioni, tukiwa bado kwenye mazungumzo na tulikaribia, Man United ikaja na Pauni 12 milioni, ikambeba.”

Ronaldo hivi karibuni alikiri kuhusu kukutana na Wenger, akisema: “Nilikutana na Arsene Wenger na ilikuwa niende Arsenal. Nilizungumza na Barcelona, Real Madrid na Inter pia, lakini mechi ya kirafiki dhidi ya Man United, ambayo ilivutiwa na mimi, ilifanya haraka ikanisajili.”

2) Lionel Messi

Kama kumkosa Ronaldo halikuwa jambo baya sana, Arsenal ilimkosa pia supastaa mwingine, Lionel Messi asicheze kwenye kikosi chake. Kiukweli, Wenger alisema kwamba dili hilo lilikuwa gumu kidogo kukamilika, lakini angeweza kumnasa Messi katika staili nyingine tofauti na kwenda kukipiga kwenye kikosi cha Arsenal.

Kumekuwa na uvumi kwamba Messi alipewa hadi jezi ya Arsenal yenye jina lake, kitu ambacho Wenger alikikataa, licha ya kukubali kuwapo kwa mazungumzo.

“Tulikuwa kwenye mazungumzo wakati tulipomsajili Fabregas,” alisema Wenger akimzungumzia Messi.

“Kipindi kile kulikuwa na makinda kama Messi, Pique na Fabregas. Pique na Fabregas walikuja England, Messi alibaki Hispania. Tulitaka kumsajili, lakini alikuwa haguswi kwa wakati ule.”

3) Jadon Sancho

Kinda Jadon Sancho atakwenda kuikamatia dunia na kuwa supastaa mkubwa kama Messi na Ronaldo? Hilo linasubiri muda. Lakini, kama ilivyo kwa Ronaldo na Messi, Sancho pia aliwahi kuwa kwenye rada za Kocha Wenger, akitaka kumsajili alipokuwa Arsenal.

“Tulitaka kumchukua kutoka Man City wakati alipokuwa hachezeshwi huko,” alisema Wenger.

“Nilitaka kumsajili kwa sababu ni mtoto wa London. Nilijaribu kumsajili ili aje Arsenal.”

Hata hivyo, jitihada za Wenger ziligonga mwamba na Sancho alikwenda kujiunga na Borussia Dortmund, mahali ambako anatamba kwa sasa na kuwindwa na timu kibao vigogo huko Ulaya.

4) Zlatan Ibrahimovic

Supastaa, Zlatan Ibrahimovic alikaribia kabisa kuwa mchezaji wa Arsenal, lakini Wenger alitibua dili hilo kwa kumtaka mchezaji huyo afanye majaribio kwanza kitu ambacho staa huyo wa Sweden aligoma na kwenda zake Ajax.

“Arsene alinipa jezi yao ile nyekundu na nyeupe, yenye namba 9 na jina la Ibrahimovic na hakika nilivutiwa hata kupiga nayo picha nikiwa nimeivaa,” alisema Ibrahimovich.

“Kilikuwa kipindi kizuri kwangu. Arsenal ilikuwa na timu nzuri wakati ule na walitengeneza jezi kwa ajili yangu tu. Na hapo nikamsubiri Wenger anishawishi ili nijiunge rasmi na Arsenal, lakini hakufanya hivyo.

“Hakutaka kunipa nafasi kwenye timu ya wakubwa, alitaka anione mimi ni mzuri kiasi gani, kwamba nifanya majaribio. Sikuamini kabisa, sikufanya, kwa sababu Zlatan hafanyi majaribio.”

Wenger alipoulizwa juu ya jambo hilo alisema: “Alikuja hapa akiwa na umri wa miaka 16, lakini akaenda Ajax, kitu ambacho kilinihuzunisha sana kwasababu nilitaka kumsajili. Najuta si tu kwa sababu nimeshindwa kumsajili akiwa mchezaji kijana mwenye kipaji, bali vile alivyokuja kujitengenezea umaarufu mkubwa Ulaya na kuwa mmoja kati ya washambuliaji bora wa aina yake.”

5) Paul Pogba

Jina jingine kubwa la mwanasoka aliyewahi kabisa kufukuziwa na Arsenal ni kiungo Mfaransa, Paul Pogba.

Kwa bahati mbaya, Mfaransa huyo alitimkia zake Juventus, mahali ambako alicheza soka la kiwango cha juu na kusajiliwa tena na Manchester United, tena kwa pesa nyingi, Pauni 89 milioni.

“Mambo yalitokea kwa haraka sana. Tulikuwa tukimtaka Pogba,” alisema Wenger mwaka 2014.

“Tulijaribu kumsajili ili aje Arsenal. Lakini, haraka alikwenda kusaini Juventus.”

Pogba kwa sasa yupo Man United, lakini bado anaweza kuondoka kwenye timu hiyo ya Old Trafford. Hata hivyo, humtarajii kama ataweza kwenda Arsenal tena kwa sasa.

6) Didier Drogba

Kwa wachezaji wote ambao Arsenal ilishindwa kuwasajili licha ya kuwataka, hakuna aliyekuwa akiwatesa zaidi kila walipokutana kama Didier Drogba. Straika huyo matata wa kimataifa wa Ivory Coast alikuwa kwenye kikosi cha Chelsea na siku zote alikuwa akiwafunga tu Arsenal kila alipokutana nao. Drogba alikuwa akichangaka sana uwanjani kila alipokutana na Arsenal.

“Nilipenda sana niwe kocha wa Didier Drogba kwa sababu mbili,” alisema Wenger.

“Nilimkosa kumsajili alipokuwa akicheza huko Ufaransa, Le Mans – sio hata kwenye ligi kubwa. Nilijua alikuwa mchezaji mzuri, lakini nilimkosa.

“Kitu cha pili, amekuwa akitufunga sana kwenye mechi kubwa na kutusababisha machungu, ambayo yasingekuwapo kama tungemsajili.”

7) N’Golo Kante

N’Golo Kante alitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji bora kabisa waliowahi kusajiliwa na Leicester City hasa ilipokwenda kumnasa kutoka Ufaransa kwa pesa ndogo sana. Lakini, kabla ya kutua King Power, Arsenal ilikuwa na nafasi ya kumchukua kiungo huyo. Lakini, Wenger alijivutavuta na matokeo yake, Kante alitua Leicester City na baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu England akatimkia zake Chelsea, alikokwenda kubeba pia taji hilo la ubingwa wa ligi.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu Kante, Wenger alisema: “Kwamba tulitaka kumsajili Kante? Ndio.

“Kipindi hicho alipokuwa Ufaransa na hata kipindi alichokuwa Leicester.”

8) Gianluigi Buffon

Wenger alikuwa na mtihani mzito katika siku zake za mwanzomwanzo huko Arsenal na mtihani huo ulikuwa kumpata mrithi wa kipa David Seaman. Baada ya kipa huyo Mwingereza kustaafu, Wenger alitafuta kipa mwingine na kwenda hata kupata kahawa na Gianluigi Buffon, kipindi hicho akiwa kinda huko Parma, lakini akionekana kabisa kuwa bora.

“Nakumbuka nilikuwa na umri wa miaka kama 20 hivi mwaka 1998, niliwahi kukutana na Wenger na kupata mlo pamoja,” alisema Buffon.

Hata hivyo, Arsenal hao hawakuwa pekee yao kutoka England kumtaka kipa Buffon, ambaye aliamua kwenda kujiunga na Juventus. Timu nyingine zilizomtaka kipa huyo gwiji wa Italia ni Man Unted, ambapo kocha wao wa kipindi hicho Sir Alex Ferguson alihangaika kupata saini yake, lakini akashindwa kabla ya Manchester City nayo kwenda kujaribu bahati yake baada ya kuwa chini ya umiliki wa matajiri wa Kiarabu.

9) Yaya Toure

Hili jambo si la kificho, Yaya Toure alifanya hadi majaribio kwenye kikosi cha Arsenal. Kiungo huyo alicheza mechi moja kwenye kikosi cha Arsenal katika kipindi chake alichokuwa akifanyiwa majaribio katika timu hiyo ya Kocha Wenger.

Wenger mwenyewe alikiri kwamba alitaka kumsajili staa huyo ambaye baadaye alikwenda kuwa mchezaji mkubwa sana kwenye vikosi vya Barcelona na Manchester City.

“Sitaki kusahamu kwamba Yaya Toure tulifikia makubaliano naye,” alisema Wenger.

“Na si kwa sababu hakutaka kumsajili ndio maana akaenda Ukraine. Tulikuwa tukisubiri hati yake ya kusafiria kutoka Ubelgiji. Tulifanya kosa, lakini halikuwa kosa na hivyo akaamua kwenda zake Metalurh Donetsk. Alikuwa akienda huko bila ya hati ya kusafiria.”

10) Luis Suarez

Wenger alimkosa Luis Suarez kizembe sana, unaweza kusema hivyo. Kwa namna alivyokwenda kutafuta huduma ya mshambuliaji huyo kutoka Liverpool ilikuwa staili ya kihuni na hapo ndipo alipojiharibia kunasa saini ya straika huyo moto, aliyetimkia zake Barcelona baadaye.

Ni hivi, kwenye mkataba wa Suarez huko Anfield ulikuwa na kipengele kinachofichua kwamba kama kuna timu itakayokuwa na uwezo wa kutoa dau linalozidi Pauni 40 milioni, basi wanamnasa. Basi alichokifanya Wenger, akapeleka Pauni 40,000,000.01 ili kumnasa mshambuliaji huyo wa Uruguay, jambo lilolowakera mabosi wa Liverpool na kuhoji kama huko Emirates wanatumia sigara yoyote inayolevya.

“Tulikuwa na makubaliano na mchezaji na tulipewa ushauri mzuri wa kuhusu kipengele kilichokuwa kwenye mkataba wake,” alisema Wenger. Kutokana na hilo, Liverpool iliamua kumuuza Suarez kwenda Barcelona mwaka uliofuatia licha ya Wenger kudai walikuwa na makubaliano ya kumsajili mshambuliaji huyo.

Barcelona nayo ililipa Pauni 75 milioni.