Taifa Stars yalazimisha sare kwa Rwanda

Muktasari:

Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya maandalizi ya  Rwanda na Tanzania kwa mechi zao dhidi ya Ethiopia na Sudan za kusaka kufuzu kwa Chan 2020 Cameron zitakazofanyika mwishoni mwa wiki hii.

Dar es Salaam. Taifa Stars ikicheza bila ya nahodha wake Mbwana Samatta imefanikiwa kulazimisha suluhu na Rwanda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa kwenye Uwanja wa Nyamirambo, Kigali.

Nahodha Samatta ameshindwa kuambatana na timu hiyo Rwanda kwa kuwa amefunga harusi yake hivi karibuni, hivyo jukumu la kuongoza mashambulizi ya Stars liliachwa kwa Saimon Msuva.

Mchezo huo wa kirafiki makocha timu hizo mbili wenyeji Rwanda na Tanzania walikuwa wakitumia katika kujianda kwao na mechi dhidi ya Ethiopia na Sudan za kusaka kufuzu kwa Chan 2020 Cameron zitakazofanyika mwishoni mwa wiki hii.

Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake kwa kuwaanzisha wachezaji wengi wapya.

Mshambuliaji Adi Yussuf alianza pamoja na Msuva katika safu ya ushambuliaji, lakini wawili hao walishindwa kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao kutokana na wenyeji Rwanda kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo hasa eneo la kiungo.

Rwanda pamoja na kutawala mchezo kwa kupiga pasi nyingi, lakini walikosa mbinu sahihi ya kuipenya ngome ya Stars iliyokuwa chini ya mkongwe Erasto Nyoni kufanya timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 0-0.

Katika kipindi cha pili kocha Ndayirangije aliwatoa Adi, Abdul Aziz Makame, Himid Mao, Farid Mussa na Msuva na kuwaingiza Ditrim Nchimbi, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Lyanga pamoja na Abdubakar Salum.

Mabadiliko hayo yalisaidia kuituliza Stars na kuanza kumiliki mpira, lakini timu hiyo ilikosa ubunifu wa kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji Nchimbi na Lyanga.

Kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu Tanzania, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere alishindwa kuonyesha makali yake hadi alipotolewa katika dakika 70, hali hiyo ilikuwa sawa na Haruna Niyonzima alishindwa kuisaidia Rwanda kupata ushindi.