Dah! Mkude ametukata mitama, tuko chini

Muktasari:

Sitaki kumzungumzia Chama. Simfahamu sana. Jonas ndiye namfahamu na nadhani ametuangusha. Pale eneo la kiungo la Simba ndiye fundi anayetegemewa na Watanzania atuwakilishe, sambamba na Hassan Dilunga.

RAFIKI yangu, Jonas Mkude na rafiki yake, Mheshimiwa Chota Chama majuzi nasikia walitoroka kambini kwenda mtaani kukata kilaji. Nimecheka sana. Kama nawaona vile Mtanzania na Mzambia walipounganisha nguvu kupambana na glasi za kilevi.
Simba wamewaita katika Kamati ya Maadili. Hili nalo litapita. Ndani ya mioyo watu wa Simba wanajua umuhimu wa Mkude na Chama. Watazuga huku na kule lakini mwisho wa siku mambo yatakaa sawa. Ndivyo zilivyo timu zetu. Nyakati fulani wachezaji mahiri wanakuwa wakubwa kuliko timu. Kama unabisha basi sawa.
Sitaki kumzungumzia Chama. Simfahamu sana. Jonas ndiye namfahamu na nadhani ametuangusha. Pale eneo la kiungo la Simba ndiye fundi anayetegemewa na Watanzania atuwakilishe, sambamba na Hassan Dilunga. Vinginevyo ni eneo ambalo wageni wamekuwa wakilitawala miaka ya karibuni.
Mkude na Dilunga wakizubaa tu nafasi zitakwenda kwa wageni. Hatuna wachezaji wengi mahiri katika vikosi vya timu zinazotumia pesa. Labda Yanga au kule Azam ambako kuna akina Salum Aboubakar. Kwa Simba, Mkude na Dilunga ndo wanatubeba. Na ndio wanaibeba pia timu ya taifa, Taifa Stars pia.
Jonas anatuangusha kwa sababu zama za mastaa kutoroka kambini kwenda kupiga kilaji zimepita zamani. Zamani akina Said Mwamba Kizota na Hamis Gaga ndio zilikuwa zao. Hata hivyo, mazingira na maisha yalikuwa tofauti.
Nyakati zile wachezaji walikuwa hawalipwi sana. Miaka ile wachezaji walikuwa sio wa kulipwa. Kuna mambo wasingeweza kuyafanya kiurahisi katika miaka hii. Siku hizi ukitazama kiasi cha pesa ambacho wachezaji wanapewa kwa ajili ya kusaini mikataba inabidi wakubali tu kujichunga. Ukiangalia mishahara yao na posho zao kwa mwezi, inabidi wakubali tu wajichunge.
Hata hili suala la kukaa kambini wachezaji wa aina ya Jonas ndio wanatuangusha. Kwa sasa hawapaswi kukaa kambini. Ilibidi wajichunge wenyewe watokee nyumbani.
Kwanini umlipe mchezaji pesa nyingi na hapo hapo umuelekeze namna ya kuishi?
Asilimia 80 na zaidi ya Watanzania hawaingizi ambacho wachezaji wetu wa Simba, Yanga na Azam wanaingiza. Inabidi waiheshimu kazi yao hata kama wanasikia kiu kikali. Ni suala la kuwaheshimu Watanzania wengine wenye vipato duni. Lakini hapo hapo tukumbushane kwamba, wachezaji hawazuiwi kukata kilaji. Wao sio mashine. Hata akina Wayne Rooney wanakata kilaji. Hata hivyo, wanatazama ratiba zao vema sana.
Kwa pesa zao za sasa, akina Mkude wamefikia hadhi ya kukodi Apartment na kufanya vurugu zao zote pindi wanapokuwa hawana ratiba ngumu. Ndivyo wanavyofanya akina Rooney. Baada ya hapo unarudi kuutumikia mpira ambao unakupa riziki kubwa.
Lakini, pia Mkude ametuangusha kwa sababu anafahamu jinsi ambavyo miaka michache iliyopita kulikuwa na wachezaji mahiri katika nafasi yake na waliimbwa sana, leo hawapo tena katika midomo ya watu. Wengine ni rafiki zake hata kama wamemzidi umri.
Anaweza kuongea tu na rafiki zake kama akina Athuman Idd ‘Chuji’ watamwambia jinsi ambavyo mpira wa Kitanzania hauna fadhila. Leo unaimbwa, unavimbishwa kichwa, unafanya matukio ya utovu wa nidhamu bado mashabiki wanakutetea, lakini mpira ukianza kupungua mguuni mashabiki hao hao wanakugeuka haraka sana.
Mbaya zaidi unajikuta hauna mpira miguuni wala pesa mfukoni. Heshima inapotea. Ndio maana wachezaji wanashauriwa kukusanya pesa na kuwekeza vema kwa sababu kazi ya soka ni ya muda mfupi. Haupaswi kufanya mambo ya ajabu.
Wakati fulani nikiwa Genk, Mbwana Samatta aliwahi kuniambia jinsi ambavyo mchezaji inabidi uachane na mambo mengi unayoyatamani kwa ajili ya kupitisha kipindi chako cha soka. Kipindi kikipita unarudia tabia zako za zamani. Katika lugha rahisi, wenyewe wanasema inabidi uyatoe kafara mambo mengi kwa ajili ya kufanikiwa jambo moja tu, la kucheza mpira.
 Kuna hili suala la kocha wa timu ya taifa, Etienne Ndayiregije kusema kwamba hatambui utovu wa nidhamu uliofanywa na Mkude pale Simba. Ettiene ni rafiki yangu. Ninachojua Mkude pia amemuangusha kocha wake wa Taifa Stars.
Ni kweli ameng’ang’ania kuwa naye kikosini kwa sababu alicheza vema katika mechi zilizopita. Hakutaka kumuacha. Kama angemuacha tungeweza kuelewa, lakini amemng’ang’ania huku akiwa amemuangusha.
Makocha wa klabu mara nyingi huwa wanatofautiana na makocha wa timu za taifa kila mmoja akijiona kiburi.
Anachofanya Etienne ni kufunika kombe Mwanaharamu apite, lakini najua atazungumza naye ni kumwambia jinsi alivyomwangusha.
Mwisho kabisa Jonas amewaangusha washikaji zake waandishi wa habari. Kama ilivyo zamani, siku hizi pia kuna urafiki mzuri kati ya wachezaji na waandishi. Kuna kundi la waandishi wanaitwa ‘Waandamizi’. Amewaangusha kwa sababu hawajui hata wamripoti vipi kamanda wao.
Ndio tatizo la kuwa staa mkubwa kama Mkude. Ukishafanya ujinga unajikuta umewaangusha watu wengi wanaokuzunguka. Achilia mbali familia yako lakini watu kama ‘waandamizi’ pia wanajikuta katika wakati mgumu kushika kalamu zao na kuandika kitu upuuzi uliofanya. Siku nyingine amkumbuke kila mtu kabla hujashika glasi.