Zahera ashituki kitu Yanga kuibuka kivingine

Muktasari:

Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wa kwanza nyumbani uliopangwa kuchezwa CCM Kirumba, jijini  Mwanza, ila tatizo kubwa la majeruhi lililopo katika timu  hiyo imeanza kuwapa hofu kwani nyota 12 afya zao zipo shakani kuwahi mechi hiyo, huku 10 kati ya hao wakiwa ni wale wa kikosi cha kwanza.

Dar es Salaam. HUKO Jangwani kwa sasa mabosi wa Yanga, wameanza mikakati mbalimbali ya kuwamaliza Waarabu wa Pyramids wanaovaana nao kwenye mechi za mchujo (play-off) ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini imebainika nyota 10 wa kikosi hicho wametishia kutibua mipango hiyo mapema.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wa kwanza nyumbani uliopangwa kuchezwa CCM Kirumba, jijini  Mwanza, ila tatizo kubwa la majeruhi lililopo katika timu  hiyo imeanza kuwapa hofu kwani nyota 12 afya zao zipo shakani kuwahi mechi hiyo, huku 10 kati ya hao wakiwa ni wale wa kikosi cha kwanza.
Mabosi wa Yanga wanalisikilizia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama litawakubalia kuhamisha mchezo huo kutoka Uwanja wa Taifa hadi Kirumba kwa kile kilichodaiwa kutokana na kuwa na mechi zao za Ligi Kuu Kanda ya Ziwa kabla ya pambano hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwanaspoti limepenyezewa, mabosi wa Yanga wanahaha kwa sasa kukabiliana na janga hilo la majeruhi na orodha ya wanawapa presha ni kama ifuatavyo;

Ali Ali, Boxer
Beki ya kulia ya Yanga kwasasa ina mtu mmoja tu aliyefiti kiafya,  Nahodha Msaidizi, Juma Abdul ila wenzake wawili wanaocheza nafasi hiyo Ali Ali na Paul Godfrey ‘Boxer  hawako sawa.
Ali aliumia katika mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Coastal Union ambao Yanga ilishinda 1-0, huku Boxer akianza mazoezi binafsi baada ya kuumia katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers na dua pekee kwa Yanga sasa ni kuomba CAF imruhusu beki wake mpya, Mustapha Seleman acheze.

Sonso naye
Upande wa kushoto nao umebaki na beki mmoja, Mharami Issa ‘Marcelo’ baada ya beki aliyecheza mechi nyingi msimu huu Ally Mtoni ‘Sonso’ naye kuingia chumba cha majeruhi, huku Jafary Mohamed akiwa mchezaji pekee anayeweza kuziba nafasi hiyo, iwapo Kocha Mwinyi Zahera ataamua kutumia plan B.
Kati ndio balaa
Mashaka makubwa zaidi yapo katika beki ya kati ambapo mabeki waliocheza mechi nyingi Lamine Moro na pacha wake mkongwe, Kelvin Yondani wote ni majeruhi. Moro ambaye hata hivyo, hatacheza mchezo wa kwanza wa Pyramids kwa sababu ya kutumikia adhabu ya kadi nyekundu, aliumia katika mchezo wa ligi dhidi ya Polisi Tanzania ulioisha kwa sare ya 3-3, huku Yondani akipata maumivu akiwa na Taifa Stars kiasi cha kushindwa kusafiri na kikosi hicho kwenda Rwanda kwa mchezo wa kirafiki utakaopigwa leo jijini Kigali.
Eneo jingine lenye majanga Yanga ni kiungo kwani Mohammed Issa ‘Banka’,  aliumia kwenye mchezo wa kwanza wa Zesco United, huku winga Patrick  Sibomana akiumia ule wa pili, ilihali mkongwe Mrisho Ngassa anayewapokea mara nyingi, naye ameumia mazoezini wiki hii.
Kwenye safu ya ushambuliaji hali nayo ni tete, kwani kama Yanga haitapata kibali cha kumtumia David Molinga basi mashaka yatakuwa makubwa baada ya Sadney Urikhob kuungana na Issa Bigirimana katika kikosi cha majeruhi wa timu hiyo.
Bigirimana ambaye alianza mazoezi baada ya kukaa nje kwa muda mrefu na kukosa karibu mechi zote inaelezwa amepata maumivu tena akiwa mazoezini wakati akijipanga kurejea huku Urikhob akipata maumivu katika mchezo wa Polisi na mpaka sasa hajaweza kurejea.
Mbali na hao pia, winga Juma Mahadhi naye bado hajatengemaa tangu apate majeraa ya muda mrefu zaidi ya msimu mmoja na nusu, huku kinda  anayetumika kama kiraka katika safu ya ulinzi Cleofas Sospeter naye ni majeruhi pia.

Kocha huyu hapa
Akizungumzia hali hiyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alikiri kwa sasa majeruhi ni changamoto kubwa kiasi hata ratiba ya mechi za kirafiki nazo zimekuwa ngumu kupangika kutokana na idadi hiyo.
Mwandila alisema tayari wameshaujulisha uongozi juu ya changamoto hiyo ambapo sasa wanasubiri majibu ya mabosi wao katika kulifanyia kazi hilo huku hali hiyo ikitibua mipango yao katika kujiandaa na mechi zote zilizopo mbele yao.
“Tumekuwa katika wakati mgumu kutokana na majeruhi hawa, sasa tuna muda wa kutosha hapa katika mapumziko ya timu za taifa lakini tunasita hata kuandaa mechi  za kirafiki mpaka jana (juzi) tulikuwa na wachezaji tisa tu wa kikosi cha kwanza.”
“Huwezi kuanza kuangalia ubora wa wapinzani wako wakati hali yako katika kikosi chako haiko sawa, tunaimani uongozi utatutafutia suluhisho la haraka katika hili linatupa wakati mgumu,” alisema.
“Tulihitaji mechi za kirafiki sasa katika muda huu lakini tunapata wasiwasi wa kuongeza majeruhi zaidi tumelazimika kuongeza idadi ya wachezaji kutoka kikosi  cha vijana ili waje kuungana na waliopo.”

Msikie Bosi wa ufundi
Naye  Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Salum Rupia alisema tayari wameshapokea changamoto hiyo ambapo hata wao imewashtua na sasa wanaanza kutafuta suluhisho la kudumu ili kulitatua jambo hilo.
Rupia alisema idadi ya majeruhi ni kubwa na ni wazi inawapa nafasi ndogo makocha kutekeleza wajibu wao na sasa uongozi wao unajipanga kwa haraka kutafuta suluhu  ya haraka kwa matibabu ya wachezaji hao.
“Tumelisikia hilo, unajua kwa sasa nimekuwa nahudhuria mazoezi ya timu na nimeshuhudia hilo, tunachofanya sasa kama uongozi ni kupambana na hilo kutafuta wapi tutapata matibabu sahihi kwa hawa vijana wetu ili warudi katika kuitumikia klabu,” alisema Rupia.