VIDEO: Shiboub atupia Simba ikiichapa Mashujaa FC

Muktasari:

Simba watacheza mchezo wao mwingine wa kirafiki dhidi ya Aigle Noir kesho kutwa Jumatano katika uwanja huo huo wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Dar es Salaam. Bao la kiungo Sharaf Shiboub limetosha kuipa Simba mwembamba wa goli 1-0 dhidi ya Mashujaa Fc katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Kiungo Shiboub aliifunga bao hilo pekee dakika 56, akiunganisha krosi iliyopigwa na Rashid Juma na kuwainua mashabiki wa Simba waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo kuishangilia timu yao.

Katika mchezo huo timu zote zilishindwa kuonyesha kiwango kizuri kutokana na ubovu wa eneo la kuchezea la Uwanja wa Lake Tanganyika.

Kikosi cha Simba, kikiongozwa na Said Ndemla ambaye alikuwa nahodha wa mchezo huo, kilianza vizuri mchezo huo licha ya kutokuwa na makali kwenye safu yao ya ushambuliaji.

 

Kocha Patrick Aussems alimuanzisha kinda, Dickson Mhilu aliyekuwa akicheza kama mshambuliaji wa mwisho huku akisaidiwa na Ibrahimu Ajibu, aliyeanza kwenye mchezo wa pili mfululizo wa kirafiki.

Rashid Juma na Francis Kahata ambao walikuwa wakitokea pembeni walionekana kudhibitiwa na mabeki wa Mashujaa ambao walikuwa wakicheza kwa ushirikiano.

Aussems alikifanyia mabadiliko kikosi chake kipindi cha pili kwa kuwatoa Kahata na Ajibu huku nafasi zao wakiingia, Deo Kanda na Sharaf Shiboub.

Mabadiliko hayo, yalionekana kuwa na faida kwa Simba dakika ya 56 baada ya Shiboub, kufunga bao la kichwa akimalizia krosi ya Rashid.

Kikosi kamili cha Simba, kilichoanza kwenye mchezo huo wa kirafiki, Aishi Manula, Athumani Mtamilwa, Joseph Peter, Yusufu Mlipili, Kennedy Juma, Said Ndemla, Rashid Juma, Maulid Lembe, Dickson Mhilu, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata.

Simba wanatarajiwa kucheza mchezo mwingine wa kirafiki kesho dhidi ya Aigle Noir ya Burundi kama sehemu ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam.