Mtibwa Sugar yajipanga kuanza ligi kwa Ndanda

Muktasari:

Mtibwa wanatarajia kuwa wageni wa Ndanda FC Oktoba 19 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema anamtihani mkubwa kuhakikisha timu yake inapata matokeo ugenini dhidi ya Ndanda ili kurudi katika hali ya ushindani.

Mtibwa Sugar imecheza michezo mitano na kuvuna pointi mbili baada ya kukubali kichapo cha michezo mitatu na kutoka sare michezo miwili.

Katwila alisema amekaa na wachezaji na kubaini hawana changamoto yoyote kilichotokea katika michezo hiyo ni sehemu ya matokeo na kubainisha kuwa sasa wanachokiangalia ni namna gani watapata matokeo ugenini.

"Tumepoteza na kutoa sare katika michezo hiyo matokeo tuliyakubali na yametupa changamoto sasa tumeyasahau tunachokiangalia ni namna ya kupata pointi kwenye michezo iliyombele yetu," alisema Katwila.

"Nina mtihani mgumu nimerudi na kujiunga na timu na natarajia kuanzia ugenini Oktoba 19 mwaka huu nitakuwa Mtwara nawaheshimu kwa sababu naenda kwenye uwanja wao wa nyumbani kikubwa tunaingia katika mchezo huo tukiwa tumetoka kujeruhiwa na kuandika rekodi mbaya katika michezo ya kwanza ya Ligi," alisema Katwila.