Miyeyusho aingia mitini raundi ya nne ulingoni Kenya

Muktasari:

Tangu Oktoba mwaka jana Miyeyusho hajapanda ulingoni kuzichapa hadi jana alipocheza nchini Kenya na kupoteza.

Dar es Salaam. Bondia Francis Miyeyusho amekubali kipigo cha Technical Knock Out (TKO) baada ya kushindwa kurudi ulingoni raundi ya nne.

Mtanzani huyo aliyezichapa usiku wa kuamkia leo Jumapili nchini Kenya pambano la uzani wa light aligoma kurejea ulingoni na kuruhusu ushindi wa TKO dhidi ya Emmanuel Chivoli.

Kocha aliyeambatana na bondia huyo, Emmanuel Mlundwa amesema Miyeyusho hakurudi ulingoni baada ya kengere ya kuashiria kuanza raundi ya nne.

"Alianza vizuri raundi tatu za awali, lakini akiwa mapumziko kusubiri raundi ya nne alipata maumivu ya misuli," alisema Mlundwa.

Awali Miyeyusho alipangiwa kucheza na George Onyango na hadi anapima uzito Ijumaa ilikuwa hivyo kabla ya mpinzani kubadilika baadae.

 "Hatujui sababu ya mpinzani wake kubadilishwa, tulijua anapigana na Onyango, lakini baadae akaja huyo aliyepigana naye" alisema Mlundwa.