Sports Charity yazindua kituo cha michezo Sabasaba Mwanza

Muktasari:

Kituo hicho ni cha pili kuzinduliwa jijini Mwanza, ambacho kinatarajia kutumia takribani Sh 180 milioni ambapo mwaka jana Taasisi hiyo ilizindua kituo cha michezo Mirongo/Nyakabungo.

Mwanza. Taasisi inayojishughulisha na masuala ya michezo jijini Mwanza, Sports Charity imesema mikakati yao ni kujenga viwanja zaidi ya 20 vya michezo baada ya miaka 10 ijayo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha michezo Sabasaba kilichopo wilayani Ilemela jijini Mwanza, Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Isack Mwanahapa amesema mkakati wao ni kujenga viwanja 20.

“Leo tunazindua mradi mwingine wa kituo cha michezo Sabasaba ikiwa ni mwendelezo na utekelezaji wa mipango yetu ya kuboresha na kujenga viwanja, tunatarajia kujenga viwanja zaidi ya 20 kwa miaka 10 ijayo,” alisema Mwanahapa.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amesema serikali itaendelea kutoa sapoti katika sekta ya michezo na kwamba kwa juhudi zinazoonyeshwa na wadau zipo dalili za Mwanza kuendelea kufanya vizuri kuliko Mikoa mingine.

“Binafsi katika kuhakikisha naunga mkono juhudi hizi nitatoa mifuko 100 ya saruji lakini serikali itakuwa pamoja na nyinyi katika kuimarisha miundombinu ya michezo hapa mkoani,” alisema Mongella.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mambula alisema kupatikana kwa kituo hicho cha michezo ni moja ya juhudi zake katika kukuza michezo wilayani humo.

“Hii ni hatua ya kwanza,zipo miradi nyingine ambayo itafika maeneo mengine kama Buswelu,Bugogwa na Kayenze,lakini kupitia michuano ya Angelina Jimbo Cup tumeweza kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la ushindani,” alisema Mabula ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo.