Hakunaga Kipchoge tema mate chini

Sunday October 13 2019

Mwanaspoti, Kenya, Tanzania, Mwanasport, Hakunaga huyo, Kipchoge tema mate chini, Mbio Dunia, Olimpiki

 

By FADHILI ATHUMANI

Nairobi. AMA kweli ‘No Human is limited’. Ndio, kimombo ni kigumu lakini kutokana na alichofanya Eliud Kipchoge, kwa kukimbia mbio za kilomita 42 ndani ya muda wa saa 1:59:40 kimethibitisha kwamba hakuna kinachoweza kumshinda mwana wa Adamu akidhamiria.
Dunia jana Jumamosi ilishangazwa na ukomo wa uwezo wa bingwa wa dunia wa marathoni na Olimpiki, Mkenya Kipchoge. Kumaliza mbio hizo kwa sekunde tisa mbele ya muda kuliishangaza dunia na waandaaji wa INEOS 1:59 Challenge.
Lakini amini usiamini, kama ulidhani ushindi huo umemshangaza Kipchoge, basi unakosea sana. Kilichomshangaza Kipchoge pamoja wachache wanaofahamu uwezo wake siyo rekodi hiyo, bali zawadi alizopewa.
Ni kwamba, kukimbia mbio hizo kwanza kabisa kunamfanya Kipchoge mwenye umri wa miaka 35 kuwa mmiliki wa ndege binafsi. Naam, mfanyabiashara bilionea Jimmy Wanjigi ameahidi kumzawadi ndege hiyo kabla ya Novemba 28.
Ushindi huo ambao ni wa kwanza kushuhudiwa unamfanya aingize mfukoni Sh8.7 bilioni kutoka kwa wadhamini INEOS, Sh97.9 milioni kutoka kampuni ya magari ya Isuzu na Sh217.5 milioni kutoka kampuni ya viatu ya NN na Nike.
Zawadi zingine ni Sh65.3 milioni kutoka kwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko; Sh43.5 milioni kutoka Kaunti ya Nandi na nyingine Sh54.4 milioni kutoka Kaunti ya Uasin Gishu bila kusahau Sh326.3 milioni kutoka kampuni ya simu ya Safaricom na ubalozi wa bidhaa za kampuni hiyo.
Kipchoge ambaye anashikilia ubingwa wa Olimpiki alitumia sekunde tisa mbele ya muda iliyowekwa na waandaaji wa mbio hizo za INEOS 1:59 Challenge, zilizofanyika jijini Vienna, Austria.

Kipchoge aushinda mkono wa muda
Kwa macho ya kawaida ya binadamu wa kawaida, mbio za IEOS 1:59 Challenge si mbio za kawaida kama ilivyo mbio zingine.
Bingwa wa dunia wa marathoni na anayeshikilia rekodi ya mbio hizo, Kipchoge ambaye ni mzaliwa wa Kapsisiywa, Kaunti ya Nandi eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya, aliuonyesha ulimwengu ukomo wa uwezo wa mwanadamu.
Achana na kampeni iliyofanyika dunia nzima kuhamasisha mbio hizo zisizotambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF). Sahau kabisa kuhusu pesa zilizomwagwa kudhamini mbio hizo. Sahau pia kuhusu furaha iliyopo kwenye mioyo ya Wakenya na Waafrika.
Tangu kuumbwa kwa dunia, imeshuhudiwa mwanadamu akipambana na mkono wa sekunde ya saa. Jiji zima la Vienna lilisimama. ‘INEOS 1:59 Challenge’ na Kipchoge kwa kweli wameonyesha ‘No human is limited’.
Akiongozwa na wakimbiaji (pace makers 41) kutoka mataifa zaidi ya 20 tofauti, bingwa huyo wa Olimpiki alianza kukata mbuga akisaidiwa na kiatu cha kipekee kilichotenengezwa maalumu (Nike ZoomX Vaporfly NEXT%), kwa ajili ya mbio hizo na Kampuni ya Nike akikimbia nyuma ya gari maalumu.
Akishindana na rekodi yake, Kipchonge alianza kampeni hiyo taratibu kuanzia saa 3:15 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki (saa moja na dakika 15 kwa saa za Austria).
Kwa kasi ileile, kilomita 20 zilimalizika ndani ya dakika 57. Dunia ikashangaa.
Hadi kufikia saa 4:44 asubuhi tayari Kipchoge alikuwa amekamilisha kilomita 31, ambapo kwa mujibu wa mkono wa muda ilimchukua saa 1:28:03 kumaliza kilomita na kubakisha kilomita 11 tu kuweka rekodi itakayotikisa dunia. Alihitaji dakika 28 kujishangaa.
Saa tano kamili asubuhi, ilimkuta Kipchoge akimalizia kilomita 34 akiwa ametumia saa 1:40:34 na kubakisha kilomita sita ambazo ni sawa na dakika 19 kuweka rekodi mpya. Kufika saa 5:10 tayari alikuwa amemaliza kilomita 39 akitumia muda wa saa 1:52:04 ambapo zilibaki kilomita 2.6 kukamilisha mbio.

Rekodi
Hatimaye lile ambalo wengi walidhani lisingewezakana liliwezekana ndani ya Jiji la Vienna.
Historia iliandikwa baada ya muda wa saa 1:59:40. Dunia itamkumbuka mwana wa Kipchoge aliyeushangaza ulimwengu kwa kuushinda mkono wa muda. Haijawahi kutokea.
Akiongozwa na timu namba 9 ya waongoza mbio ambayo iliundwa na Wakenya watatu, bingwa huyo wa dunia anayeshikilia rekodi ya marathoni na ubingwa wa Olimpiki, alivuka utepe sekunde tisa kabla ya ya muda uliowekwa.

Kipchoge anasemaje
Baada ya kumaliza mbio hizo alipoulizwa anajisikiaje, Kipchoge hakusita kumshukuru Mwenyezi Mungu huku akisisitiza kwamba, kama kuna siku aliwahi kuwa katika wakati mgumu ni dakika chache kabla ya saa 3:15 (2:15 saa za Vienna).
“Nashukuru Mungu kwa kufanikisha ndoto hii, kama nilivyosema awali hakuna binadamu asiyeweza kufanya maajabu, kila mtu ana uwezo wa kufanya atakalo akijiamini….kabla ya saa mbili na robo, nilikuwa katika wakati mgumu sana, nadhani nilikuwa na mchecheto,” alisema Kipchoge.

Ugumu wa njia
Vienna ipo mita 150 kutoka usawa wa bahari, wakati ambapo Eldoret ambako ndiko iliko kambi yake ya mazoezi ni mita 2000 kutoka usawa wa bahari.
Maana yake ni kwamba, hali ya hewa ya Eldoret ilisaidia sana kufanikisha ushindi wa Kipchoge.
Mbali na hali ya kijiografia ya Vienna, waandaaji ambao ni Ineos, Kampuni ya Nike na Sir Ratcliffe walihakikisha wanachagua njia yenye barabara tatu tofauti ambayo ingemsaidia kumkinga na dhoruba ya upepo.
Njia hiyo ilinyooka kwa asilimia 90. Hiyo ilimsaidia kukimbia kwa kasi zaidi.
Kongole kwa mwana wa adamu Kipchoge. Kwa mara ya kwanza mwanadamu ameushinda mkono wa muda. Historia imeandika na itabaki kukumbuka jina la Kipchoge.

Ruto awaongoza Wakenya kushuhudia maajabu
Makamu wa Rais wa Kenya, Dk William Ruto alikuwa miongoni mwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza jijini Vienna kumshuhudia bingwa wa dunia wa rekodi ya mbio za marathon, Kipchoge akiushinda mkono wa muda.
Dk Ruto ambaye ni mpenzi mkubwa wa riadha alionekana kwenye mstari wa watazamani wa kawaida akifuatilia mbio hizo ambazo zilimalizika kwa Kipchoge kuishangaza dunia, alipoweka rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kumaliza kilomita 42 ndani ya saa 1:59:40.
Mara baada ya mbio hizo kumalizika, ikiwa sekunde tisa mbele ya muda uliowekwa wa saa 1:59:49, Dk Ruto alikuwa wa kwanza kwenda kumpongeza

Uhuru, Raila waungana kumpongeza Kipchoge
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga waliwaongoza Wakenya kumpongeza, bingwa huyo wa marathoni baada ya kuweka rekodi hiyo.
Kabla ya kuanza kwa mbio hizo, Rais Kenyatta alimpigia simu Kipchoge moja kwa moja na kumtakia kila la heri, huku akiahidi kumpigia pindi atakapomaliza mbio hizo.
“Nitakupigia ukimaliza ndugu yangu, Mungu akubariki, utafanikiwa lakini kwetu siyo mafanikio katika kuvunja rekodi, bali pia kule tu kuthubutu ni mafanikio, kila la heri ndugu yangu,” alisema Rais Kenyatta.
Kupitia akaunti yake ya Twitter, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Odinga, aliandika: “Hata kabla ya kuanza kwa mbio hizi, tayari ulikuwa umeishangaza dunia, ulichokifanya ni zaidi ya uthubutu na ushujaa, Kongole sana kwa kumaliza mbio chini ya saa mbili. Kenya imepata sifa.”Advertisement