Goodluck Gozbert ameyatimba ‘Big time’ kupanda jukwaa la Fiesta!

Muktasari:

Kamusi mpya ya muziki iliyoletwa Bongo ni mwanamuziki wa nyimbo za Injili, Goodluck Gozbert, kupanda jukwaa la Fiesta na kugonga shoo pamoja na wakali wa nyimbo za kidunia. Eti hapo anatoa huduma. Dunia ina mambo hii!

Dar es Salaam.Katika kamusi ya muziki, tuna wauza dawa za kulevya waliogeuka wanamuziki na kutoboa; mchukue Notorious BIG, Jay Z na 50 Cent kama mfano. Wapo wengine wengi! Kuna wanamuziki wa nyimbo za kidunia walioamua kufanya kazi ya Mungu; Mzee Yusuf, Cosmas Chidumule, Remy Ongala, K Basil na wengineo!

Hata Aman, yule mdada fundi muziki wa Kenya, aliyeimba “Bad Boy”, tukaambiwa ni shemeji yetu kwa Mzee wa Commercial ‘AY’, naye siku hizi anaimba nyimbo za kusifu na kuabudu. Ester Wassira aliyetuimbia ‘Sheila’ na akabamba, naye ni mtumishi wa Mungu siku hizi!

Katika muziki, ipo kamusi mpya imeletwa Bongo. Kabla ya kwenda huko, ngonja nikumbushe; Mwaka 1999, kipindi rapa Mase akiwa wa moto, pesa zinamkimbilia, akitambulika ndiye staa namba moja pale Bad Boy Records ya P Diddy, akaona maisha ya dunia sio mpango. Akasema anakwenda kumtumikia Mungu. Mase akawa mchungaji!

Miaka mitano baadaye, yaani 2004, Mase alirejea kwenye Hip Hop. Ikabainika kuwa alipokwenda kwenye utumishi wa Kanisa, alianza kufulia. Kilichomrudisha Mase kufanya Hip Hop, sio kingine ni pesa. Hapo ni uamuzi wako ‘kubet’ kuwa alikimbilia benjamins kanisani, alipozikosa, akazirudia katika Hip Hop. Ni hivyo tu, hutachana mkeka!

Kamusi mpya ya muziki iliyoletwa Bongo ni mwanamuziki wa nyimbo za Injili, Goodluck Gozbert, kupanda jukwaa la Fiesta na kugonga shoo pamoja na wakali wa nyimbo za kidunia. Eti hapo anatoa huduma. Dunia ina mambo hii!

Nyimbo ambazo Goodluck anaimba zina sura ya kujenga watu matumaini na kuwapa moyo kuwa nyakati ngumu za kimaisha zinavukwa kwa kumtegemea Mungu. Angeweza kuziimba akijiita M’Bongo Fleva na isingekuwa na shida yoyote. Angepanda jukwaani Fiesta, wala kusingekuwa na mshangao wowote.

R Kelly si ndio tunamwita mfalme wa R&B? Ana nyimbo nyingi za kutukuza ukuu wa Mungu na uponyaji, huyo Goodluck wenu hafikii hata ukucha. Toka “Prayer Changes” hadi “U Save Me” au alivyompa maujiko mrembo mchamungu aliyembadilisha akawa mtu mwema katika “Religious”. Endelea na Storm is Over, I Surrender na nyingine kibao kujaza albamu kadhaa, lakini R Kelly hakuwahi kujitangaza kuwa mwanamuziki wa nyimbo za Injili. Hata sasa na kesi zake za ‘unyambilisi’ wa kimapenzi kwa watoto wadogo, hasemwi mwanamuziki wa Injili mwenye kashfa za ngono. Ni R Kelly wa R&B. Period!

Shida ya Goodluck ni kile cheo alichojipa. Injili ni andiko tukufu. Injili ni maandishi ya Mungu ndani ya kinywa na matendo ya Yesu. Kama kwa Uislam, Kuran ni maneno ya Mungu kupitia mdomo na maisha ya Mtume Muhammad. Sawa na Zaburi kwa Daud, vilevile Torati ya Musa.

Huwezi kusema unafanya utumishi kwenye jukwaa la Fiesta wakati ukishuka wewe jukwaani anapanda Mario anaimba “Chibonge” halafu uwanja mzima unalipuka “anatikisa minyama tu, akipita minyama tu”. Kweli hapa hakuna utani?

Anapanda jukwaani Goodluck na nyimbo zake akidai anataka kuitibu jamii, halafu akishuka anapanda Joh Makini anasema “agizia kina Ritha Margaritha, usijifanye kama hujui kilichotuleta, mawaidha kwenye party hapana kuleta”, na uwanja mzima unashangilia.

Kabla ya Joh na baada ya kushuka Goodluck, Jux aliwaimbisha wote “napenda unavyokata na kunipa taratibu, me ni mgonjwa, we ni dokta unanitibu, nikikushika unanitazama unaona aibu, we tabibu, unanipa raha”.

Ujumbe gani ambao Goodluck anataka kuufikisha? Kwamba neno la Mungu liliisha nguvu baada ya wanamuziki wa nyimbo za kidunia kupanda jukwaani? Mzani wa nyimbo za starehe umesheheni kuliko wa nyimbo za kumtukuza Mungu?

Goodluck anawachongea Watanzania kwa Mungu, kwamba hawaeleweki wanataka nini? Alipopanda yeye walimfurahia kuonesha wanakubali nyimbo za kumpa sifa Muumba, kisha ilipofika zamu ya watu wa nyimbo za matendo, furaha ikapaa?

Labda Goodluck aseme kuwa aliamua kushiriki matamasha ya Fiesta 2019 ili kupima msuli wake ni kwa kiasi gani nyimbo zake zimeweza kubadilisha jamii ya Kitanzania. Au alikusudia kuiambia jamii kwamba nyimbo za Injili zinabamba kuliko za kidunia. Kama ndivyo, basi amefeli sana. Amefeli big time!

Lazima kutofautisha maneno “Secular Music” na “Sacred Music”. Sacred ni nyimbo za utukufu wa Mungu kwa dini yeyote. Secular ni nyimbo za kidunia. Wahenga wa Kilatini mwanzoni mwa Karne ya 12, waliziita nyimbo za Secular kwa jina “Chansom de Geste”, yaani nyimbo za matendo.

Mzee Yusuf, zamani alikuwa mtawala wa muziki wa Taarab, kwa hiyo alifunika kwenye nyimbo za matendo (secular), ila baada ya kutubu, siku hizi anaimba Kaswida (sacred). Na Kaswida ni nyimbo za utukufu wa Mungu na kumpa daraja Mtume Muhammad (S.A.W).

Jinsi Mzee Yusuf alivyomwaga machozi siku alipofanya toba msikitini pale Ilala, halafu siku moja apande jukwaa la Fiesta na kuimba Kaswida, Joh Makini atamfunika kwa shangwe atakaporap “mawaidha kwenye party hapana kuleta”. Rostam watambagaza na wimbo wao “Mwajuma Kaolewa”.

Goodluck akubali mambo yafuatayo, kwamba alikubali kupanda Fiesta kwa lengo la kifedha na sio kutoa huduma ya kiroho. Akiri kuwa ufanisi wake Fiesta haukuwa wa kitumishi, bali wa kimatendo. Zaidi alikosea kuiimbia nyimbo za kumsifu Mungu, hadhira ambayo haikuwa imeandaliwa kwa mapokeo. Hadhira ya Fiesta ni ya party. Wahusika wao ni akina FID Q, Nandy, Aslay na kadhalika.

Ni kama kanisani au popote kwenye shughuli ya Kanisa, aalikwe Nay Wamitego na kuimba “Nakula Ujana”, Dully Sykes aitwe msikitini au hafla yoyote ya Kiislam, atumbuize “Bombadia”. Utani uwe pembeni.

Ni hivi Goodluck ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, sema aliona fursa katika jukwaa la nyimbo za Injili, akatoboa. Ni vizuri aheshimu jukwaa lililompokea na kumtunuku nyota alizonazo. Kama inampendeza na anaona Bongo Fleva kuna pesa kuliko Injili, na kwake pesa ni kwanza kabla ya huduma, atangaze kurejea, mbona Mase aliacha uchungaji akarudi kwenye Hip Hop? Kuimba Injili kwenye Fiesta sio poa! Ameyatimba ‘big time’.