Huko Gor Mahia ni msoto buda, mabosi watembeza bakuli

Muktasari:

Gor wana miezi miwili tangu walipowalipa wachezaji wao mishahara yao na sasa ukiwa unaingia mwezi wa tatu, uongozi uameanza kuhaha. Hata zaidi, Gor wana hofu ya kimaandalizi ya mchuano wao wa marudio dhidi ya USM Alger waliowalima mabao 4-1 ugenini.

MSOTO unaendelea kuwatesa Gor Mahia na sasa wamejigeuza ombaomba huku wakiwa na kibarua kizito wikendi hii.
Gor kwa sasa wanahitaji kiasi kisichopungua Sh12 milioni ili kulipa mishara ya wachezaji wake pamoja na kujiandaa kwa mechi ya marudio ya CAF Champions League dhidi ya USM Alger ya Algeria wikendi hii.
Gor wana miezi miwili tangu walipowalipa wachezaji wao mishahara yao na sasa ukiwa unaingia mwezi wa tatu, uongozi uameanza kuhaha. Hata zaidi, Gor wana hofu ya kimaandalizi ya mchuano wao wa marudio dhidi ya USM Alger waliowalima mabao 4-1 ugenini.
Kulingana na ofisa mkuu mtendaji wa Gor, Lordvick Aduda, mabingwa hao mara 18 wa Ligi Kuu ya Kenya wanahitaji Sh10 milioni kwa ajili ya kulipa deni ya mishahara ya wachezaji wake.
Kisha wanahitaji Sh2 milioni kugharimia maandalizi ya mechi hiyo ya marudio dhidi ya USM Algers iliyoratibiwa kuchezewa katika Uwanja wa Kasarani Jumapili ya wiki hii.
“Kikweli sasa hivi tunaumia vibaya sababu tumesota kinoma. Tuna mechi Jumapili dhidi ya USM Alger inayohitaji gharama, pia tunadaiwa na wachezaji wetu mishahara ya miezi miwili. Hatuna fedha kabisa,” Aduda kakiri.
Kulingana na ofisa huyo, Gor wakiwa wenyeji wanatakiwa kugharimia nauli za ndege za maofisa wanne watakaosimamia mechi hiyo ambayo ni Sh500,000.
Pia wanatakiwa kuwabukia hoteli na kugharimia msosi wao pamoja na usafiri wa ndani kwa siku nne watakazokuwepo nchini. Vile vile watahitaji kiasi kisichopungua Sh300,000 kuwalipa maofisa hao wanne mishahara yao ya shughuli hiyo watakayopiga Jumapili.
Gor pia ndio wanaopaswa kugharimia usafiri wa wapinzani wao kutoka uwanja wa ndege hadi hotelini mwao, pia kwenda uwanjani. Pia watahitaji Sh300,000 kulipia Uwanja wa Kasarani.
“Hizi ndizo hesabu tulizonazo na kama unavyoona kuandaa mechi nyumbani pia ni gharama sawa tu na kusafiri kwa mechi za ugenini,” Aduda kaongeza.
Mpaka sasa Gor hawajua watakakotoa hela hizo huku wakigeuka ombaomba na kuwarai mashabiki wake kuwasaidia na michango ili waweze kupata hela hizi lau sivyo wataishia kupigwa faini nzito na CAF.
Jipya hili linajiri wiki chache tu baada ya Gor kuhangaika tena kupata Sh5 milioni kugharimia nauli zao za ndege kwenda Algeria kwa ajili ya mechi ya ugenini. Waliandaa mchango uliochangisha Sh1.5 milioni pekee kabla ya kuokolewa na serikali iliyogharimia tiketi za wachezaji 16.
Gor wamejikuta katika hali hii tangu mdhamini wake mkubwa Sportpesa alipositisha udhamini wake kutokana na kupokonywa leseni ya kufanya biashara na serikali.