Polack: Tunachapa Waarabu Kasarani

Muktasari:

Gor wanaruadiana na Mwarabu US Algers Jumapili  ya wiki hii uwanjani Kasarani baada ya kulimwa kule kwao mabao 4-1 na hivyo kuwaweka pabaya.

HUKU mashabiki na wadau wengi wakiwa tayari wameshakata tamaa ya Gor Mahia kufuzu kwa hatua ya makundi ya dimba la CAF Champions League, Kocha Steven Polack angali mwingi matumaini watayapindua matokeo.
Gor wanaruadiana na Mwarabu US Algers Jumapili  ya wiki hii uwanjani Kasarani baada ya kulimwa kule kwao mabao 4-1 na hivyo kuwaweka pabaya. Wadau wengi wanasisitiza Gor hawawezi kuyapindua matokeo hayo hasa kutokana na hali ya kifedha wanayopitia kwa sasa ikiwa imewavuruga akili lakini kubwa zaidi ikiwa  idadi hiyo kubwa ya mabao.
Hata hivyo, kocha huyo Mwingereza anasisitiza Gor sio timu ya kwanza kuwahi kushuhudiwa ikitoka nyuma na kupindua matokeo, hivyo ni jambo linalowezekana sana.
“Mpango wangu ni kuwaongoza wasifungwe bao katika kipindi chote cha mchezo na kwa wakati huo wajitahidi kadri ya uwezo wao kupachika mabao hasa katika kipindi cha kwanza,” Pollack anasema.
Hata hivyo, hofu yake ni mbinu watakazohitaji kutumia kujilinda huku wakishambulia, kutokana na mtindo wa uchezaji wa Waarabu.
“Haitakuwa kibarua rahisi sababu ninavyoelewa timu za Kaskazini mwa Afrika hucheza soka la kimashambulizi zaidi jambo ambalo linaweza kutupa presha sana tutakapokuwa tukijaribu kudifendi na kwa wakati huo tukifanya mashambulizi. Pamoja na yote tutahitaji kujitahidi,” Pollack kaongeza.
Kikwazo kingine alicho nacho Kocha Pollack ni ukosefu wa wachezaji nyota ambao wengi wapo nje kutokana na kuwa majeruhi.
Beki wa kulia Philemon Otieno ana jeraha la goti alilopata akiwa na timu ya taifa kule Misri kwa ajili ya AFCON. Mpaka sasa hajaweza kutibiwa akiwa anahitaji kufanyiwa upasuaji. Kiungo Ernest Wendo pia yupo nje kutokana na jeraha hali sawia na Curtis Wekasa, straika tegemeo Nicholas Kipkurui pamoja na Ghislain Yikpe.
Licha ya majeraha hayo, Pollack kasema ana kikosi kikubwa cha wachezaji 26, hivyo hawezi kushindwa kupanga kikosi bora cha First 11 kutoka kwa timu hiyo.