Ngorongoro Heroes yaichakaza Zanzibar Chalenji

Muktasari:

Kwa matokeo hayo, Ngorongoro Heroes na Kenya ndizo zilizofuzu kundi B huku Zanzibar na Ethiopia zikiaga mashindano hayo.

Dar es Salaam.Timu ya Taifa ya Vijana Tanzania Bara chini ya miaka 20 'Ngorongoro Heroes' leo imeichakaza Zanzibar kwa mabao 5-0 katika mashindano ya Kombe la Chalenji U-20 yanayoendelea nchini Uganda.

Mshambuliaji Kelvin John alifunga mabao matatu huku mengine yakifungwa na Lusajo Mwaikenda na Novatus Dominic.

Kelvin alifunga mabao yake katika dakika ya 51, 87 na 90+1, huku Mwaikenda na Dominic wakihitimisha kalamu hiyo ya Ngorongoro Heroes dhidi ya ndugu zao wa Zanzibar.

Katika mchezo huo, timu ya Zanzibar ilikua ikitafuta ushindi ili iweze kufuzu robo fainali baada ya kuwafunga Ethiopia bao 2-1, juzi ikishika nafasi ya tatu kundi B, huku Ngorongoro wakiwa tayari wamefuzu hatua hiyo baada ya kuwafunga Ethiopia mabao 4-0 kabla ya juzi kutoa sare ya 2-2 dhidi ya Kenya.