Bandari ‘full mzuka’ kuimaliza US Ben Kombe la Shirikisho ya CAF

Muktasari:

Kuhusu hali ya afya ya wachezaji, Shikanda alisema wanasoka wote wako sawa na kikosi kitakachokwenda huko Tunisia kitawakilisha nchi kwenye mashindano hayo

MOMBASA. USHINDI wa bao 1-0 waliopata Bandari FC dhidi ya Sony Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) imewapa morali na maandalizi mazuri wachezaji wanaoelekea huko Tunisia kuvaana na US Ben Guardane kwenye mechi ya Caf Confederation Cup, Jumapili hii.
Akiongea kuhusu mechi hiyo, Naibu Kocha wa Bandari FC, Ibrahim Shikanda alisema bao la haraka walilolipata lilitosha kuwaongezea pointi tatu, pia ilikuwa mechi iliyowapa fursa ya kurekebisha makosa madogomadogo kabla ya pambano lao na Gaurdane.
“Tumejiandaa vya kutosha na namshukuru sana Kocha Mkuu Bernard Mwalala kwa anavyowaandaa vijana wetu mechi moja hadi nyingine na viongozi wa klabu kwa jinsi wanavyoshughulikia maslahi na mahitaji ya timu hiyo,” akasema Shikanda.
Mkufunzi huyo alisema kuwa wanatarajia kuonyesha mchezo wa hali ya juu na ana materajio makubwa ya timu kupata ushindi dhidi ya Watunisia hao. “Tuna imani kubwa ya kusonga mbele kwenye dimba hili la barani Afrika,” akasema.
Kuhusu hali ya afya ya wachezaji, Shikanda alisema wanasoka wote wako sawa na kikosi kitakachokwenda huko Tunisia kitawakilisha nchi kwenye mashindano hayo. “Vijana wetu watacheza kufa au kupona dakika 90 kuhakikisha tunapata ushindi,” akasema.
Wakati huo huo, wapenzi wa soka wa Mkoa wa Pwani wameipongeza Bandari FC jinsi inavyoendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu pamoja na mashindano ya barani Afrika huku wakitaka wadhamini wa timu hiyo kujitolea kuwasafirisha mashabiki kwenye mechi za ugenini.
“Tunaomba KPA ifanye kila iwezekanavyo kuhakikisha mashabiki wanasaidiwa kwa njia za usafiri kwenda kuishangilia timu yao inapocheza mechi zao huko bara zikiwemo zile za Nairobi na kwengineko,” alisema shabiki Abdulhalil Salim.