Oliech ajisalimisha Bandari, Wazito

Muktasari:

Kocha Mwalala kaendelea kusisitiza safu yake ya mbele inahitaji kumakinika hata zaidi.
Sasa hili tatizo la uchache wa magoli , ndiyo Oliech anaamini yeye ndio tiba endapo moja kati ya klabu hizo zitaitikia kumpa kazi.

STRAIKA wa zamani wa Gor Mahia, Dennis Oliech ambaye kwa sasa anavutana na klabu hiyo baada ya kuvunjiwa mkataba, kaomba kazi katika klabu za Wazito FC na Bandari FC.
Oliech ambaye tangu avunjiwe mkataba kashindwa kupata timu nyingine ya kujiunga nayo, kaomba mojawapo ya Wazito au Bandari kumsajili ili aweze kuwasuluhishia tatizo kubwa walilonalo kwa sasa ambalo ni ufungaji mabao.
Kwa mechi ya tatu sasa wikendi iliyopita, Wazito walioutimia zaidi ya Sh8 milioni kuwasajili zaidi ya wachezaji 10, walishindwa kupata bao walipochuana na AFC Leopards na kuishia kulimwa bao 1-0.
Kwa upande wao Bandari, wamekuwa wakihangaika sana kupata mabao, hata hivyo, katika siku za hivi karibuni safu ya mashambulizi ya kocha Bernard Mwalala imeonyesha kufufuka na sasa wanapata mabao japo sio mengi kama ambavyo ingetakiwa kuonekana.
Wikendi waliwalaza Bandari waliwalaza Sony Sugar bao 1-0 wakifuatisha ushindi huo na mwingine dhidi ya Zoo Kericho wiki iliyopita, walikotoka nyuma mabao mawili na kushinda 3-2.
Kabla ya Zoo, Bandari vile vile walijizatiti kwenye mechi ya CAF Champions League na kuwalima Ben Guardene wa Tunisia mabao 2-0.
Licha ya mabadiliko hayo Kocha Mwalala kaendelea kusisitiza safu yake ya mbele inahitaji kumakinika hata zaidi.
Sasa hili tatizo la uchache wa magoli , ndiyo Oliech anaamini yeye ndio tiba endapo moja kati ya klabu hizo zitaitikia kumpa kazi.
“Nipo tayari kuendelea kucheza baada ya kupona jeraha langu la mkono. Naziona klabu kama Wazito na Bandari zinavyohangaika kupachika mabao, nipo tayari kuzisaidia. Pengine watakuwa wanasita kunitokea kwa hofu nitaisha dau kubwa, jamani eeh mimi nipo tayari kuzisikiza ofa walizo nazo ikiwa wanazihitaji huduma zangu” Oliech kasema.