Ngorongoro Heroes yafuzu robo fainali Chalenji

Muktasari:

Ngorongoro Heroes itashuka tena uwanjani Alhamis kucheza na Zanzibar Heroes wakati Kenya itaikabili Ethiopia.

Dar es Salaam.Mshambuliaji wa Ngorongoro Heroes, Andrew Simchimba amefunga bao na kuiongoza Tanzania kufuzu kwa robo fainali yamashindano ya Kombe la Chalenji kwa Vijana U20, baada ya kulazimisha sare 2-2 na Kenya.

Matokeo hayo yanaifanya Tanzania, Kenya kufuzu kwa robo fainali kabla ya mechi zao za mwisho dhidi ya Zanzibar na Ethiopia.

Kenya inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne sawa na Tanzania wakitofautiana kwa idadi ya mabao.

Chipukizi Simchimba baada ya kufunga mabao matatu katika mchezo wa awali leo amefunga bao lake la nne la mashindano hayo.

Mabao hayo manne yanamfanya Simchimba kuingia katika orodha ya vinara wa ufungaji pamoja na mshambuliaji wa Kenya, Sydney Lokale aliyefunga idadi hiyo ya magoli.

Awali Lokale aliyekuwa akiongoza baada ya kufunga mabao manne katika mchezo ambao Kenya waliichapa Zanzibar mabao 5-0, wakati Simchimba kabla ya mchezo wa leo alikuwa na mabao matatu aliyofaunga katika mchezo dhidi ya Ethiopia mabao Ngorongoro Heroes ilishinda mabao 4-0.

Timu zote mbili zimetinga robo fainali ya mashindano hayo baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo uliofanyika leo Jumanne mchana kwenye Uwanja wa Gulu Uganda.

Katika mchezo huo Kenya ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 26 lililofungwa na Otieno Odhiambo kabla ya Andrew Simchimba kusawazisha dakika ya 37.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika  ya 52 Kenya ilipata bao la pili dakika ya 52 kupitia kwa Otieno Patrick kabla ya Ngorongoro Heroes kusawazisha dakika ya 56 kupitia kwa Abdul Suleiman.

Sare hiyo imeifanya Kenya kuongoza Kundi B ikiwa na pointi nne sawa na Ngorongoro Heroes lakini zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kundi A, Uganda inaongoza ikiwa na pointi nne sawa na Sudan, lakini zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa wakati Eritrea iko nafasi ya tatu ikwia na pointi mbili na Djibout inashika mkia.

Kundi C linaongozwa na Burundi yenye pointi nne ikifuatiwa na Sudani Kusini iliyo na pointi moja wakati Somalia haina pointi.

Ngorongoro Heroes itashuka tena uwanjani Alhamis kucheza na Zanzibar Heroes wakati  Kenya itaikabili Ethiopia.