Zahera aanza kuonja joto la jiwe Yanga

Muktasari:

Mabosi wa Yanga walitaka kujua kupotea kwa washambuliaji kama Juma Balinya na jinsi safu yao ya ushambuliaji inavyoweza kuwapa matokeo katika mchezo ujao dhidi ya Zesco.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameanza kuonja joto la jiwe ndani ya klabu hiyo baada ya kuweka kitimoto na viongozi wa klabu hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika ndani ya klabu ya Gymkhana, jijini Dar es Salaam kilitumia saa tano kikianza saa 8 mchana na kumalizika saa 12 jioni, kilibeba hoja nzito mbili, ubora wa kikosi hicho sambamba na jinsi ya uimara wake kuelekea mchezo dhidi ya Zesco.
Ingawa mabosi wenye mamlaka walikuwa wazito kuzungumzia kilichojiri kwa uwazi, lakini Mwanaspoti linajua Zahera alieleza madhaifu na ubora wa kikosi chake baada ya mabosi wake kutaka maelezo ya kiufundi yanayoinyima ushindi timu hiyo nyumbani.
Aidha mabosi hao walitaka kujua kupotea kwa washambuliaji kama Juma Balinya na jinsi safu yao ya ushambuliaji inavyoweza kuwapa matokeo katika mchezo ujao dhidi ya Zesco.
Hata hivyo, inaelezwa mabosi hao walitambua benchi lao kuhitaji muda zaidi lakini hawakuonyesha kuridhika na  jinsi safu hiyo inavyopoteza nafasi katika mechi zao.
“Tulikutana naye, unajua mechi inayokuja ina umuhimu sana sasa wenye dhamana ni sisi kama viongozi, kutambua hilo tulihitaji kukutana na kocha kufahamu ubora wa timu yetu na baada ya kuulizana tukafahamishwa na kocha (Zahera) yale tuliyotaka kupata majibu kwa niaba ya wanachama,” alifichua bosi mmoja.
“Sio kwamba haturidhiki na timu yetu, hapana kuna mambo ambayo tuliona yanapigiwa kelele na mengine kuyaona wenyewe yanachangamoto hasa timu kufunga mabao mengi na ubora hata wa baadhi ya wachezaji pia.”
Alisema kutokana na hilo ndio maana wakaamua kuitana faragha ili kujadili namna ya kuwamaliza wapinzani wao ambao wana rekodi za kufanya vizuri kwenye Uwanja wa nyumbani wa Levy Mwanawasa.

Hoja ya Balinya
Aidha mabosi hao walifikisha kilio cha mashabiki wao kutoonekana kwa mshambulaji Juma Balinya na waliridhika na majibu ya Zahera huku akiwahikikishia sasa yuko sawa na atarejea katika mchezo wa marudiano.
Balinya kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika wiki iliyopita nchini, alianzia benchi wakati Yanga ikilazimishwa sare ya 1-1 na Wazambia waliochomoa bao dakika za jioni kupitia Thabani Kamusoko na kuwatibua makocha kwa vile ndiye aliyefunga bao la ushindi kwenye mechi yao ya marudiano na Township Rollers mjini Gaborone na walitarajiwa angeanza.
Hata hivyo, Zahera alinukuliwa saa chache baada ya pambano hilo, aliamua kumwacha balinya nje kwa vile alionekana kuwa mzito tangu wakiwa kambini Mwanza kujiandaa na mchezo huo, lakini kwa sasa ameonekana kuimarika na anaweza kumtumia kama alivyonukuliwa kigogo huyo wa Yanga aliyeombwa kuhifadhiwa jina.

Zahera ajitundika
Inaelezwa katika kikao hicho Zahera aliwaondoa wasiwasi mabosi wake akiwaambia kikosi chake kinakwenda kufanya kitu tofauti mjini Ndola nchini Zambia Septemba 28 dhidi ya Zesco.
“Jambo zuri kocha ana imani na timu yake ametuambia anachofahamu yeye anakwenda kushinda kulekule Zambia, hicho kikiwa sawa ni furaha yetu na kiu ya kila mwanachama sasa tusubiri tuone, ila tunaamini tutarejea yale ya Botswana,” alisema kiongozi huyo.
Katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alidokeza timu itaondoka kesho asubuhi kutua Lusaka kisha baada ya mazoezi ya siku tano, timu itaenda Ndola kwa mchezo wao ambao utaamua hatma ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa ama kutupwa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya playoff.