VIDEO: Matukio 16 yaliyotikisa dunia ndani ya siku 815 za Aveva, Kaburu wakiwa mahabusu

Sunday September 22 2019

Matukio 16, yaliyotikisa, Mwanaspoti, Tanzania, dunia, siku 815 za Aveva, Kaburu wakiwa, mahabusu

 

By CHARLES ABEL

Dar es Salaam. Baada ya kusota rumande kwa zaidi ya siku 815, Rais wa zamani wa Simba, Evance Aveva na aliyekuwa makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kesho Jumatatu wanatarajiwa kurudi uraiani kama watakidhi masharti ya dhamana  waliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Aveva na Kaburu walilazimika kusota rumande katika kipindi hicho chote wakishitakiwa kwa makosa zaidi ya nane yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo kisheria hayana dhamana.
Hata hivyo, Ijumaa mchana Aveva na Kaburu walikuwa mahakamani wakijaribu kutimiza masharti ya ili kurudi uraiani, Lakini walikwama kwa vile upande wa mashtaka kuwakatia rufaa, hivyo dhamana iliyo wazi hatma yake itakuwa Jumatatu.
Katika kipindi hicho cha siku 815 ambazo wawili hao walikuwa ndani, kuna matukio na mambo mengi ya kisoka na michezo yametokea ndani na nje ya nchi ambayo pengine kama wangekuwa nje, labda wangeweza kushiriki au kuwa sehemu ya matukio hayo.
Mwanaspoti linakuletea mtiririko wa matukio hayo ya kimichezo, kisiasa, kijamii au yanayohusiana na hayo ambayo yametokea pindi Aveva na Kaburu walipokuwa ndani.

Vifo vya wadau, wasanii
Wapo baadhi ya wadau wa michezo na burudani pamoja na wasanii maarufu ambao, wametangulia mbele za haki katika kipindi chote ambacho Aveva na Kaburu walikuwa ndani.
Mfano wa hao ni Mzee Reginald Mengi, Ruge Mutahaba, Agnes Masogange, Godzillah, Mzee Majuto, Ramadhan Nassib, Ephraim Kibonde, Isaack Gamba na Oliver Mtukudzi.

Mugabe ang’oka madarakani, afariki
Baada ya kudumu madarakani kwa muda wa miaka 37 ambayo aliiongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1980, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe aliondolewa rasmi madarakani Novemba, 2017.
Nafasi hiyo ilirithiwa na aliyewahi kuwa Makamu wake wa Rais, Emmerson  Mnangagwa ambaye ameendelea kuwa Rais wa nchi hiyo mpaka sasa. Siku chache kabla ya mambo kubadilika kwa Kaburu na Aveva, Mugabe aliaga dunia Septemba 6 huko Singapore alikokuwa akitibiwa tatizo la tezi dumeUfaransa bingwa Dunia, Ureno Ulaya
Fainali za Kombe la Dunia zilifanyika mwaka jana nchini Russia, ambapo timu ya Taifa ya Ufaransa ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Croatia mabao 4-2 kwenye mchezo wa fainali.
Mwaka mmoja uliofuata, Ureno ilitwaa ubingwa wa mashindano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya baada ya kuichapa Uholanzi kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa Fainali uliochezwa Juni 9.

Simba yatwaa mataji
matano
Aveva na Kaburu waliingia rumande wakiwa wameiacha Simba ikiwa imetwaa ubingwa wa Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup), baada ya kuifunga Mbao FC kwa mabao 2-1 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma mwezi Mei.
Hata hivyo, katika kipindi chote walichokuwa ndani, Simba imeweza kutwaa mataji matano ambayo ni ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili kwenye msimu wa 2017/2018 na 2018/2019 huku pia ikitwaa Ngao ya Jamii mara tatu ambapo ni mwaka 2017, 2018 na mwaka huu.

Ajibu aenda Yanga,
arudi Simba
Katika dirisha kubwa la usajili mwezi Agosti 2018, Simba ilimpoteza mshambuliaji wake kipenzi, Ibrahim Ajibu ambaye aliangukia mikononi mwa watani wao wa jadi Yanga ambako alitumikia kwa misimu miwili na kuwa staa wa kikosi huku akiteuliwa kuwa nahodha.
Hata hivyo, baada ya mkataba wake kumalizika, Ajibu aliwapa mkono wa kwaheri Yanga na kuamua kurejea Simba ambako ndiko alikoibukia, akiwa ni zao la kikosi cha vijana cha timu hiyo kilichokuwa kikilelewa na Kaburu.

Tanzania yafuzu Afcon
Tangu iliposhiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), Tanzania haikufuzu tena mashindano hayo kwa miaka 39 hadi ilipofanikiwa kufanya hivyo mwaka huu pindi zilipofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.
Katika Fainali hizo Algeria ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Senegal bao 1-0 kwenye mechi ya Fainali.

Simba wapitisha mabadiliko, wafanya uchaguzi
Agosti 2018, wanachama wa Simba walipitisha rasmi mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo na kuamua iwe chini ya mfumo wa kampuni ambapo mwekezaji ambaye ni Mfanyabiashara Mohamed Dewji, iliamriwa atawekeza kwa asilimia 49 huku wanachama wakiwa na umiliki wa hisa 51%.
Kana kwamba haitoshi, mwezi Novemba 2018, Simba ilifanya uchaguzi wake mkuu wa kwanza ikiwa chini ya mfumo mpya ambapo Swedi Nkwabi alichaguliwa rasmi kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo huku wajumbe wakiwa ni Mwina Kaduguda, Asha Baraka,  Hussein Kitta, Dr Zawadi Kadunda na Selemani Haroub.
Hata hivyo, kabla ya hata kurejea uraiani watashangaa kusikia kuwa, Mkwabi tayari amejiuzulu nafasi hiyo baada ya kudaiwa kiutofautiana na mwekezaji, Dewji, licha ya mwenyewe kukiri ni majukumu yake binafsi yaliyomuondoa kwenye nafasi hiyo hivi karibuni.

Simba robo fainali Afrika
Kaburu na Aveva wamekuwa sehemu ya mafanikio ya Simba kwa nyakati kadhaa lakini bahati mbaya kwao, hawakushuhudia neema ya Simba kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita wa 2018/2019.
Simba ilitinga hatua hiyo baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D nyuma ya Al Ahly ya Misri lakini ikakwama mbele ya TP Mazembe baada ya kutolewa kwa matokeo ya jumla ya kipigo cha mabao 4-1.

Yanga yatinga makundi Shirikisho
Baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018, Yanga iliangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambako iliweza kutinga hatua ya makundi lakini ikamaliza ikiwa mkiani kabisa huko.
Pia kwa kipindi chote, ambacho kina Aveva wakiwa ndani, Yanga imekuwa ombaomba kwani mwezi mmoja kabla ya kutiwa mbaroni kwa vigogo hao wa Simba, aliyekuwa Bilionea na mfadhili mkuu wa Yanga, Yusuf Manji alijiuzulu na kuifanya Yanga iyumbe.
Kuyumba huko kiuchumi kuliifanya Yanga ipoteze taji lao la ubingwa, lakini pia kutembeza bakuli, huku aliyekuwa Kocha Mkuu wao, George Lwandamina kutimika kwao.

Yanga yapata uongozi mpya
Mwezi Mei 2019, Yanga ilifanikiwa kufanya Uchaguzi Mkuu ambapo Dk. Mshindo Msolla aliibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti huku Fredrick Mwakalebela akishika nafasi ya makamu mwenyekiti.
Hii ni baada ya waliokuwa viongozi wa klabu hiyo akiwamo Clement Sanga, Boniface Mkwasa kuachia ngazi katika nafasi zao za Umakamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa klabu kisha kufuatiwa na wajumbe wa kamati ya Utendaji na kulazimisha uchaguzi.
Uchaguzi huo uliojaa mizengwe ambao awali ulikuwa wa kuziba nafasi za waliojiuzulu ulizua mzozo na kuifanya serikali kuingiilia kati na kuitishwa mkuu ambao kina Msolla na Mwakalebela walishinda katika nafasi za juu.
Upande wa wajumbe wa kamati ya utendaji, walioshinda walikuwa ni Hamad Islam, Injinia Mwaseba, Dominick Albinus, Kamugisha Kalokola, Arafat Haji, Salum Ruvila, Saad Khimji na Rodgers Gumbo

Wambura arejea na kung’olewa TFF
Wiki kadhaa tangu kina Aveva watiwe mbaroni, ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo Wallace Karia alimrithi Jamal Malinzi, huku Michael Wambura akirejea kwa kishindo kwenye uongozi wa soka akiwa Makamu wake.
Hata hivyo, Wambura alijikuta akiundiwa zengwe ndani ya TFF na kung’olewa kwa makosa ya ukosefu wa maadili na kisha kufikishwa mahakamani ambapo, mpaka sasa anasota rumande akituhumiwa kwa makosa ya utakatishaji wa fedha.

Samatta atakata Ulaya
Kipindi kina Aveva wameswekwa rumande, nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta tayari alishakuwa amesajiliwa KRC Genk ya Ubelgiji, lakini kwa kipindi chote baada ya hapo nyota huyo wametakata nchini humo na Ulaya.
Samatta mbali na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya Ulaya, lakini pia alinyakua tuzo ya Mchezaji Bora  wenye asili ya Afrika na kubeba taji la Ulebgiji na sasa wanaweza kumkuta akikunikisha Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo wiki hii aliandikisha rekodi nyingine kadhaa ikiwamo wa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano hiyo na kufunga kwenye mchezo wao wa kwanza.

Azam, Simba, Yanga zabadili
makocha
Kina Aveva kama watarejea uraiani watazikuta klabu za Simba, Yanga na Azam zikiwa na makocha tofauti na ilizowaacha nazo kipindi wakidakwa na kufikishwa mahakamani.
Wakati wakitiwa rumande Simba ilikuwa chini ya Kocha Msaidizi, Masoud Djuma, lakini kwa siku hizo zaidi ya 800 Simba imeshafudishwa na makocha watatu akiwamo Masoud, Pierre Lechantre na wa sasa Patrick Aussems. Yanga nao iliachana na Hans Pluijm na kukabidihiwa George Lwandamina aliyetimka na sasa ipo mikononi mwa Mkongoman, Mwinyi Zahera, wakati Azam iliachwa na Aristica Cioaba, lakini washapita Han Pluijm, Meja Abdul Mingange na sasa ipo kwa Etienne Ndayiragije ambaye walimuacha akiwa Mbao FC.
Hata hivyo, Ndayiragije keshapita KMC kabla ya kutuma Azam, huku Jackson Mayanja aliyeondoka Simba chini ya uongozi wa kina Aveva kwa sasa amerejea akiinoa KMC, ambayo imepanda na kushiriki michuano ya kimataifa.

Za Majeshi zabadilishwa
Yapo mengi ambayo kina Aveva watakutana nayo uswahili, lakini kubwa ni kubadilishwa kwa timu za majeshi ambapo Polisi Morogoro ikirejea tena Ligi Kuu,  kwa sasa inafahamika Polisi Tanzania, huku Oljoro JKT ikibadilishwa majina mara mbili kutoka Oljoro hadi Arusha United na kisha sasa kufahamika kama Gwambina FC.
Pia, kina Aveva watashangaa kusikia African Lyon ilipanda daraja na kushuka, huku Stand United walioachia Ligi Kuu kwa sasa ikiwa Daraja la Kwanza baada ya kushuka, sambamba na kuikuta Biashara United  iliyokuwa Polisi Mara) na Alliance zikiwa katika ligi hiyo.
Pia wanashangaa kusikia Coastal iliyoshuka kipindi chao ikirejea Ligi Kuu na mkoa wa Lindi kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi ikipata timu ya ligi hiyo, Namungo FC, mbali na kushangaa kumuona Obrey Chirwa aliyewasumbua akiwa Yanga akikipiga Azam sambamba na Donald Ngoma, huku Tambwe akiwa keshasepa zake Umangani.

Yanga yarudi kwenye neema
Kina Aveva wanarudi uraiani huku wakiikita Yanga ikirejea kwenye neema baada ya kupata mdhamini mpya wa GSM, huku wakifanya yao kwenye mechi za kimataifa ambapo Tanzania inaongezewa idadi ya timu wawakilishi kutoka mbili hadi nne na wao kung’ara.
Simba ilikwamia robo fainali msimu uliopita safari hii wataikuta ikiwa mtaani baada ya kutolewa mapema kwenye Ligi ya Mabingwa sambamba na KMC baada ya Wamakonde wa UD Songo kutoka Msumbiji kuwatibulia, huku Yanga na Azam zikipambana kusaka kuingia makundi.

Azam yabeba mataji kibao
Wakati kina Aveva wanaswekwa rumande tayari walikuwa wanajua Azam ndio mabingwa wa Mapinduzi 2017 kwani, timu yao ya Simba ilitunguliwa kwenye fainali, pia walikuwa wanafahamu Azam ni Mabingwa wa Kombe la Kagame 2015, lakini sasa wakirejea wanaikuta Azam ikiwa imeongeza idadi ya mataji hayo.
Kwanza imetwaa mara mbili mfululizo Kombe la Mapinduzi 2018 na 2019 kisha kutetea taji la Kagame tena 2018 kuonyesha siku 815 walizokuwa rumande walipitwa na mambo mengi mbali na mabadiliko kadhaa ya viongozi wa kiserikali katika utawala wa Awamu ya Tano, kupigwa risasi kwa Tundu Lissu na kwenda kutibwa nje ya nchi na akiwa bado hata harejea toka matibabuni, tayari kiti chake cha Ubunge kule Singida kikiwa kimechukuliwa, huku wabunge kadhaa waliowaacha wakiwa upinzani akiwamo Edward Lowassa wakiwa wamesharejea CCM na kuendeleza mambo yao.

Advertisement