Chelsea, Liverpool hapatoshi leo Darajani

Muktasari:

Liverpool imeshinda mara moja tu katika mechi 12 za mwisho ilizocheza ugenini kwa timu nyingine za Big Six, Chelsea, Arsenal , Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur. Ushindi huo ilikuwa Septemba 2018 walipoichapa Spurs 2-1 kwao. Katika mechi hizo, Liverpool imetoka sare mara sita na kuchapwa mara tano.

London, England. Namba hazidanganyi, lakini Jurgen Klopp anajipiga kifuani na kusema hajali na wala haogopi kitu.
Ni hivi, namba zenyewe ni kuhusu rekodi ya mechi za ugenini za kikosi chake cha Liverpool inapocheza na wababe wenzake wa Big Six kwenye Ligi Kuu England. Kwa kifupi tu, rekodi ya mechi za ugenini za Liverpool anapocheza na wababe wenzake kwenye ligi ni majanga. Huwa wanapigwa tu.
Leo, Jumapili, Liverpool watawafuata Chelsea huko Stamford Bridge wakiwa kileleni kwenye msimamo wa ligi kwa pointi kibao, huku wakitaka kuendeleza moto wao wa kushinda mara 14 mfululizo kwenye ligi. Lakini, licha ya mwanzo wao mzuri wa kushinda mechi zote tano za kwanza kwenye ligi hiyo, kocha Klopp na chama lake la Liverpool wanakwenda Stamford Bridge huku rekodi zikiwakataa kabisa wanapocheza ugenini kwa wababe wenzao.
Liverpool imeshinda mara moja tu katika mechi 12 za mwisho ilizocheza ugenini kwa timu nyingine za Big Six, Chelsea, Arsenal , Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur. Ushindi huo ilikuwa Septemba 2018 walipoichapa Spurs 2-1 kwao. Katika mechi hizo, Liverpool imetoka sare mara sita na kuchapwa mara tano.
Klopp alikiri kwamba takwimu hizo zinampasua kichwa na kumpa sababu ya kufikiri, lakini wala haogopi sana akiamini mambo yatakuwa tofauti kuanzia huko Stamford Bridge.
Kisha kocha huyo aliwazungumzia makinda wa Chelsea, Tammy Abraham na Mason Mount kuwa ni moto kwelikweli na kukifanya kikosi hicho kinachonolewa na Frank Lampard kufikirisha unapokwenda kukabiliana nazo. Lakini, kuhusu kushindwa kupata ushindi kwenye mechi za ugenini za Big Six, Klopp alisema wala hafahamu kile ambacho kimekuwa kikitokea ndani ya uwanja.
“Sifahamu kabisa kinachotokea kwenye hizi mechi, ina ninachojua tulikaribia kabisa kushinda mechi zote hizo. Nakumbuka kwa mfano ile mechi ya Arsenal, wala sifahamu Virgil van Dijk kwanini hakutumia akili kufunga baada ya mipira yake ya kichwa kugonga mwaka,” alisema.
Hata hivyo, Liverpool wanaamini hilo limeshapita na huu ni msimu mpya, hivyo kila kitu kipo tofauti na ndio maana hata msimu uliopita walibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu England, Liverpool ilipokwenda Stamford Bridge kuwakabili Chelsea matokeo yalikuwa sare ya 1-1, Daniel Sturridge alipochomoa bao la Eden Hazard katika dakika ya 89.
Ligi Kuu England iliendelea jana Jumamosi kwenye mechi kadhaa, ambapo huko King Power, Leicester City walitokea nyuma kuwachapa Tottenham Hotspur 2-1 na hivyo kupata hadi kwenye nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Hata hivyo, hiyo ilikuwa kabla ya mechi nyingine. Mabao ya Ricardo Pereira na James Maddison yalitosha kwa Leicester City kuichapa Spurs, ambayo ilikuwa imetangulia kwa bao la Harry Kane kwenye kipindi cha kwanza. Leicester sasa wamefikisha pointi 11 baada ya kucheza mechi sita, huku Spurs wakibaki na pointi zao nane. Mechi nyingine, Man City walikipiga na Watford wakawachapa 8-0, Burnley wakaipiga Norwich City 2-0, huku Everton wakipigwa 2-0 nyumbani mbele ya Sheffield United.