Tukuyu Stars, African Sports, Toto Africans kuwasha moto SDL Novemba

Thursday September 19 2019

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1986, Tukuyu Stars, pamoja na African Sports, Toto Africans ni miongoni mwa timu 22 za Ligi Daraja la Pili (SDL) zinazosaka kupanda Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Tukuyu Stars iliweka rekodi mwaka 1986, baada ya kupanda daraja na kwenda moja kwa moja kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu wakati huo ikitwa ligi daraja la kwanza, itaanza kurusha karata yake Novemba 2, katika ligi hiyo iliyogawanywa katika makundi matatu.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TBLB, Boniface Wambura kwenda kwa klabu za Ligi Daraja la Pili, kundi litakuwa na timu nane (8) wakati kundi B na C kila moja litakuwa na timu saba (7).

"Napenda kukufahamisha kuwa Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu tajwa itaanza Novemba 2, 2019 na itachezwa katika makundi matatu," inafafanua barua hiyo.

Jiji la Dar es Salaam limetikisa ligi hiyo kwa kuwa na idadi kubwa ya timu ambapo lina jumla ya timu nne huku mikoa ya Dodoma na Tabora kila mmoja ukiwa na timu tatu.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kundi A litakuwa na timu za African Sports ya Tanga, Dar City, Eagle Star na Villa Squad (Dar es Salaam), Kiluvya United (Pwani), Mbuni FC (Arusha), Mkamba Rangers (Morogoro) na Mpwapwa United (Dodoma).

Advertisement

Kundi B litakuwa na timu za Area C na Fountain Gate (Dodoma), DTB Bank (Dar es Salaam), Majimaji Rangers (Lindi), Mtwivila (Iringa), The Mighty Elephant (Ruvuma) na Tukuyu Stars (Mbeya).

Kundi C litakuwa na timu za Kitayosce, Mgambo Shooting na Milambo (Tabora), Bulyanhulu (Shinyanga), Kasulu Red Star (Kigoma), Toto Africans (Mwanza) na Usalama (Manyara)

Advertisement