Yondani, Nyoni wanogesha mazoezi ya Taifa Stars

Muktasari:

Taifa Stars inakibarua cha kuing'oa Sudan ili kupata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani maarifu kama CHAN.

Dar es Salaam. Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', kimejikita leo katika mazoezi ya utimamu wa mwili na mbinu kujiandaa na mchezo wa CHAN dhidi ya Sudan.

Katika mazoezi hayo, yaliyokuwa yakisimamiwa na kaimu kocha mkuu wa kikosi hicho, Etienne Ndayiragije kwenye uwanja wa Boko Veteran walianza kwa kupasha joto mwili kama ilivyoada kisha kujikita katika program iliyoandaliwa.

Ndayiragije akiwa na wasaidizi wake Juma Mgunda na Seleman Matola, waliugawa uwanja katika vizingiti sita ambayo vilitumika kama vituo, wachezaji wawili, kila mmoja akiwa upande wake walianza kukimbia kwa kasi katika vituo husika.

Iliwachukua dakika 10 kila mchezaji alionekana jezi yake kujawa jasho mithiri ya mtu aliyemwagiwa maji, kadri muda ulivyokuwa ukisogea ndipo kasi ya ukimbiaji kwa wachezaji hao ulivyokuwa ikipungua.

Walionekana kumudu vyema mbio hizp kwenye vituo husika, miongoni mwao ni mabeki, Kelvin Yondani wa Yanga na Erasto Nyoni wa Simba.

Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, viligawanywa vikosi viwili na kuanza kufanyia kazi namna kadhaa za uchezaji kwa kufuata maelekezo maalum kutoka kwa Ndayiragije.

Ndayiagije alionekana kutafuta muunganiko wa wachezaji wake kutokana na kikosi kimoja kujaa wachezaji ambao wamekuwa wakianza kikosi cha kwanza.

Upande golini alikuwa Juma Kaseja, beki wa kulia alikuwa Haruna Shamte,  kushoto,  Mohammed Hussein 'Tshabalala' huku mabeki wa kati wakicheza Nyoni na Yondan.

Viungo, Jonas Mkude, Salum Abubakar 'Sure boy' na Mzamiru Yassin huku mawinga wakiwa Idd Seleman 'Nado' na Hassan Dilunga, mshambuliaji alikuwa Shaaban Chilunda.