Coutinho arusha kijembe kimtindo Liverpool, Barcelona

Muktasari:

Staa huyo aliachana na Barcelona kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi akienda kujiunga na Bayern Munich kwa mkopo, lakini kabla ya hapo kocha Jurgen Klopp wa Liverpool aliambiwa kama anamtaka mchezaji huyo amchukue, lakini akagoma kufanya hivyo.

MUNICH, UJERUMANI. KIUNGO wa Kibrazili, Philippe Coutinho amedai maisha ya Bayern Munich kwake yamekuwa kama familia zaidi kuliko hata kwenye timu mbili alizopita huko nyuma, Liverpool na Barcelona.
Staa huyo aliachana na Barcelona kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi akienda kujiunga na Bayern Munich kwa mkopo, lakini kabla ya hapo kocha Jurgen Klopp wa Liverpool aliambiwa kama anamtaka mchezaji huyo amchukue, lakini akagoma kufanya hivyo.
Bayern walitoa Pauni 7.6 milioni kwa mkopo wa msimu mzima wa mchezaji huyo na kwamba watalipa mishahara yake yote kwa kipindi hicho atakachokuwa akikipiga kwenye kikosi chao.
Coutinho, 27, ameonekana kutulizana kwa haraka kwenye maiahs ya Ujerumani, ambapo ameshacheza mechi tatu za Bundesliga katika kikosi hicho hadi sasa. Mwenyewe alisema anaona Allianz Arena pamekuwa na mapokezi mazuri kwake kuliko hata muda wake wa miaka mitano aliyodumu kwenye kikosi cha Liverpool na kucheza zaidi ya mechi 200.
"Ndani ya siku hizi chache zilizokuwa hapa na kuonyeshwa mazingira, nimekutana na wachezaji wenzake na makocha. Kila siku najisikia vizuri sana, nina furaha. Bayern pamekuwa kama familia zaidi kuliko klabu zangu za zamani," alisema Coutinho.
Kocha Klopp alikiri kwamba kikosi chake kiliamua kuachana na Coutinho wakati walipopewa nafasi ya kumrudisha Anfield staa huyo, akisema kwamba amemshauri mchezaji huyo aende Bayern ndiko kunakomfaa zaidi. Klopp alisema: "Nilimwambia Bayern patakuwa bora zaidi kwake. Ni mchezaji wa kiwango cha dunia na hakika ni usajili bora kwa Bayern na Bundesliga."