Emery aruhusu mastaa wake kula bata, kujipoza

Thursday September 19 2019

Emery aruhusu, Tanzania, Mwanaspoti, mastaa wake, kula bata, kujipoza

 

LONDON, ENGLAND. KOCHA Mkuu wa Arsenal, Unai Emery amewapa ruhusa wachezaji wake kuwa na mtoko wa pamoja kwenda kula bata akiwataka kutuliza vichwa vyao baada ya kile walichokipata kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Watford Jumapili iliyopita.
Staa Pierre-Emerick Aubameyang aliyeonekana kuwa na hasira kwa matokeo ya sare ya 2-2 kwenye mechi hiyo dhidi ya Watford, ambapo Arsenal walitangulia kufunga mara mbili, kisha mabao yote yakarudi, alionekana akitoka kwenye ukumbi mmoja wa starehe za usiku huko Mayfair asubuhi ya Jumatatu.
Ripoti zinadai kwamba kocha Emery alitoa ruhusa hiyo kwa wachezaji wake kutoka kwenda kumpumzisha vichwa baada ya matokeo hayo ya Jumapili.
Jumatatu ni siku ya mapumziko kwa wachezaji wa Arsenal, lakini baadhi ya mashabiki walimtaka kocha wao kufuta 'off' hiyo ili wafanye mazoezi kutokana na kiwango cha hovyo kabisa walichokionyesha kwenye mechi ya Jumapili.
Straika Aubameyang alifunga mara mbili ndani ya dakika 32 na kuwaweka Arsenal kwenye njia nzuri, lakini ya kufanya makosa yaliyowagharimu na Watford wakisawazisha yote huko wakifanya mashambulizi hatari ambayo yalimweka Emery kwenye wakati mgumu na hofu ya kupoteza mechi. Katika mchezo huo mabeki wa Arsenal, Sokratis na David Luiz walifanya makosa, mmoja akisababisha bao la kwanza lililofungwa na Tom Cleverley na mwingine akisababisha penalti baada ya kumwaangusha Roberto Pereyra ndani ya boksi. Watford walikuwa na nafasi ya kushinda kama si kiungo Abdoulaye Doucoure shuti lake kumlenga kipa Bernd Leno katika dakika za mwisho.
Arsenal leo Alhamisi watakuwa na kibarua cha kuwakabili Eintracht Frankfurt kwenye Europa League kabla ya wikiendi kuja kucheza na Aston Villa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Kocha Emery yupo kwenye kitimoto na ripoti zinadai kwamba huenda akapigwa chini.

Advertisement