UD Songo imekatisha ndoto mapema ya Gadiel kucheza Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Gadiel alikuwa mchezaji wa pili kutoka Yanga kuhamia Simba kama ilivyokuwa kwa Ibrahim Ajibu na wote waliondoka kama wachezaji huru baada ya kumaliza mikataba yao.

Dar es Salaam. MOJA ya silaha mpya ndani ya kikosi cha Simba msimu huu ni beki wa kushoto, Gadiel Michael ambaye alitua kwa wekundu hao akitokea kwa watani wao Yanga.
Gadiel alikuwa mchezaji wa pili kutoka Yanga kuhamia Simba kama ilivyokuwa kwa Ibrahim Ajibu na wote waliondoka kama wachezaji huru baada ya kumaliza mikataba yao.
Kujua maisha yake ndani ya Simba na jinsi alivyoamua kuhamia upande wa pili, Mwanaspoti lilimtafuta na kufanya naye mahojiano maalumu.

MAISHA YA SIMBA     YAKOJE?
“Maisha ya Simba yako vizuri, kila kitu kipo sawa kama kawaida, nashukuru nilipokelewa vizuri na viongozi na wachezaji wenzangu. Pia nashukuru maisha yanasogea tukiwa kama kundi lenye malengo sawa.”

USHINDANI WA NAMBA
“Kila kitu lazima ujiandae, kwa maana ya ushindani sehemu yoyote utakayokwenda lazima uwe ujiandae nami ndivyo ilivyo, kwani hata nilipotoka ushindani ulikuwepo.”
“Tshabalala ni beki mzuri kama mimi, namkubali sana lakini tumekutana Simba ili kuisaidia klabu muhimu kwangu ni kumshawishi mwalimu katika kila nafasi nitakayopata,” anaongeza.

AUSSEMS AMPA MZUKA
Katika msimu wake wa kwanza ndani ya Simba atakuwa na Kocha Patrick Aussems, hapa anaelezea alichoambiwa na bosi wake anachokitaka:
“Ukiacha kunikaribisha anataka mtu anayejituma na kucheza kwa nidhamu ya mchezo, hayo yote sio mambo mapya muhimu ni mimi mwenyewe kuweka umakini na kujituma, ndio maana ameendelea kuniamini ligi bado ina safari ndefu.”

CHANGAMOTO SIMBA HADI TAIFA
Ushindani wa namba kwa Gadiel haupo klabuni tu, bali hadi katika timu ya taifa, Taifa Stars ambako naye ni miongoni mwa nyota wa timu hiyo naye anafunguka alipoulizwa anakabiliana vipi na changamoto hizo;
“Muhimu ni kuwa na malengo katika safari ya namna hiyo lazima changamoto ziwepo, kuweza kucheza katika klabu na timu ya taifa sio kitu chepesi. Unahitaji kuwa na ubora mkubwa, nafikiri mpaka sasa nafikisha mechi 36 tayari nina uzoefu.”

VIPI AWEKWAPO BENCHI?
“Mchezaji lazima ukue kiakili, haijalishi umeanza au umeanzia benchi ukiwa benchi wewe ni sehemu ya mchezo, ukiwa benchi si kwamba, hujui kocha anakuwa na maana yake. Angalia kama mechi ya Stars ya mwisho hapa nyumbani na Buru ndi mb ona hapa nilia nzia benchi na baadaye nikaingia, lakini ukirudi nyuma mchezo wa kwanza nilianza na kucheza vizuri. Hii ina maana kocha ana lengo lake, mimi naamini kila kitu makocha wanakuwa na mipango yao na maana yao.”

KUHAMA         HAKUJAMSUMBUA?
“Siku zote kama mchezaji lazima ujiamini, nilipokuwa nahama nilisema kikubwa natakiwa kupambana huku ninakokwenda, muhimu nilijipa moyo najua na najiamini sasa acha nifanye maamuzi ya kwenda Simba,” anasema Gadiel kwa kujiamini.
Hata hivyo, anakiri haikuwa kazi rahisi kufanya maamuzi hayo ikizingatiwa Yanga walikuwa wakimhitaji.

LINALOSUMBUA KICHWANI
Gadiel anafichua kitendo cha kuhama kilimsumbua kichwa, japo kwa sasa anajiona freshi.
“Nakumbuka siku chache kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho niliumia sana kichwa haikuwa siku nzuri, kuna wasiwasi unakuja maswali kichwani yanakuwa mengi lakini nashukuru mwishowe nilimtanguliza Mungu na nikaamua.”

YEYE NA YANGA FRESHI TU
Alipoulizwa kama kuhama kwake kumemfanya azinguane na watu wa Yanga na pengine kumnyima raha, Gadiela anasema; “Sababu kubwa iliyonifanya nihame ni kutafuta changa moto mpya na ndani yake katika sababu hiyo ni masilahi tu hakuna kitu kingine. Unajua nimefanya kazi Yanga sikuwahi kugombana na yeyote tangu nilipoingia nilifanya kazi yao kwa weledi mkubwa na nawashuru kwa ushirikiano wao na sasa maisha yangu na akili yangu ipo Simba.”

SIMBA SIO BAHATI MBAYA
Beki huyo aliyeolea jijini Tanga anafichua, kutua kwake Simba wala sio kwa bahati mbaya kabisa kwa kufunguka hivi; “Kusema ule ukweli baada ya kucheza Yanga sikuwa na akili nitacheza tena Tanzania, nilikuwa na ndoto ya kucheza nje ya nchi na kama utakumbuka miezi michache nyuma niliyoenda kufanya majaribio nje ya nchi lakini mambo hayakwenda sawa kama nilivyotarajia na baadaye ikaja dili ya Simba nikafanya maamuzi.”

MKEWE AMTAITI, ILA AKAELEWA
“Mke wangu ni mtu muhimu kwangu kwa sasa, kwani tunashauriana mambo mengi, alijua mpango yangu mingi sasa hata nilipokuja kumwambia la kuhamia Simba, awali alinipiga maswali, kwanini nimeamua hivyo. Maswali yake yalikuwa na maana kwani kuna mambo tulishayapanga awali, ila nashukuru baadaye nilivyomuelewesha alielewa na kunipa nguvu ya kumalizia maamuzi hayo ambayo yamenifanya niwe Msimbazi.”

MIPANGO IPO KIBAO
Alipoulizwa ana mipango gani nje ya Simba kwa sasa nayeb hakuwa na hiyana kw kujibu;
“Nipo Simba, lakini ukweli ni kwamba bado natamani kucheza nje ya Tanzania, kwa sasa nina mkataba na Simba napaswa kuweka nguvu sana hapa, ila katika hilo nitahakikisha kazi yangu inakuwa biashara kwa klabu zingine za nje kuhitaji huduma yangu.”
“Najua tumeshatoka katika mashindano ya kimataifa ambayo yalikuwa na maana kubwa katika malengo yangu nilikuwa nahitaji na nimepanga vitu vingi, lakini tayari hatupo tena muhimu ni kuweka nguvu kujituma katika mashindano yaliyosalia.”

HAKULALA KUNG’OLEWA CAF
Simba katika hatua ya kushtusha iliondolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuipa UD Songo ya Msumbiji faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 hapa nchini kumbe Gadiel aliumia sana na hapa anaeleza;
“Niliipokea vibaya sana ile mechi baada ya matokeo, usiku mzima sikulala niliteseka sana ni kama nilikuwa naota kumbe ni hali halisi imetokea.
“Nakumbuka kesho yake tulikuja mazoezini, lakini hali yangu ilikuwa mbaya sana niliona kama kuna kitu kimepungua katika maisha yangu kama nilivyosema nilikuwa na malengo mengi na kuna mawakala wa klabu mbalimbali walikuwa wananifuatilia sana,” anasema.

ANAYEMSUMBUA
“Hapa Tanzania sidhani, lakini kwa wenzetu waliotoka, Simon (Msuva) yule jamaa ni noma. Huyu tangu nikiwa Azam alikuwa ananisumbua sana ana kasi na mjanja sana, anajua lakini nje kuna Mahrez (Riyad) yule mtu ni habari nyingine hatulii ukimtoa nje anakusumbua ukimleta ndani ndiyo kabisa yule mtu anajua buana we acha.”

BIASHARA AMA UDEREVA MALORI
Alipoulizwa kama sio soka alitarajiwa kuwa nani, naye akaanika ukweli kwa kusema kuwa;
 “(Anafikiria kidogo) Isingekuwa soka, nahisi ningekuwa mfanyabiashara kwani napenda sana fani hiyo, yaani biashara yoyote au pia ninge kuwa pia nae ndesha malori kazi ambayo kaka yangu anaifanya mpaka sasa, hata baba yangu mzazi aliwahi kuifanya huko nyuma.”