Ni kweli ndoa ya Lulu na Majay inasubiri daftari la mpigakura

Muktasari:

Mwenyekiti wa kamati, akatajwa bosi wa Dar, Paul Makonda. Siku hizi jiiii! Swali; kwani na ndoa ya Lulu na Majizzo inangoja daftari la mpigakura, iandikishwe ndio ifungwe?

WAKATI fulani ‘ishu’ ya ndoa ya supastaa Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Majay a.ka.a Majizzo ilibamba. Tukasikia vikao vimeanza. Mwenyekiti wa kamati, akatajwa bosi wa Dar, Paul Makonda. Siku hizi jiiii! Swali; kwani na ndoa ya Lulu na Majizzo inangoja daftari la mpigakura, iandikishwe ndio ifungwe? Luqman Maloto na Dk Levy wapo ‘streit-fowad’.
LUQMAN: Hivi Dk Levy kwani utaniambia nini?
LEVY: Nitakuambia nini bana nyie Team SimZesco. Lazima mtambe kama mlivyotamba Makiriri walipotoa dro Daslama mjini.
LUQMAN: SimZesco ndo nini?
LEVY: Muulize Manara wenu. Unajua watu wanaosambaza umeme makusudi, dawa yao kutumia kinga na usilete ufundi mwingi. Zesco ni wasambazaji wa umeme kule kwao. Nadhani unaelewa umeme maana yake nini kwa lugha za Mwananyamala.
LUQMAN: Mpaka hapo sijaelewa unataka kwenda wapi. Tengeneza ‘topic’ kwanza, Zesco wamekufanya nini?
LEVY: Nataka kwenda Ndola niwashangaze na Team Vipensi. Nyinyi mtaendelea kuzurura mitaa ya Msimbazi kama wauza vijora. Sisi ni mwendo wa anga kwa anga kama mawaziri wa masuala ya kigeni.
LUQMAN: Mpaka hapo hata sijakuelewa. Kuvaa pensi na goli la Kamusoko kuna uhusiano wowote?
LEVY: Taratibu unajipambanua kama vile watu wasiojulikana. Uchawi ni asili yenu na fitina ni jadi yenu. Unafki mlifunga nao ndoa.
LUQMAN: Mimi ni kati ya watu ambao tulimuwinda Kamusoko na bakora, akaniponyoka. Tumemlea wenyewe hapa Bongo, lakini akatufunga ‘mgoli’ ule, tena katika dakika zile za kosa la marehemu, kwani wewe Kamusoko hakukudhi?
LEVY: Hajaniudhi ila siku nikikutana naye ndo utaelewa namtafakari vipi. Mtu mpaka lugha ya kiswahili tumemfundisha hapa hapa. Kibaya sio lile kombora kama la yule mtu mbaya wa  Senegal kwa Manula, bali kushangilia kinoko vile tena kwa staili ya mwamba wetu Heritier Makambooooooo... Makambovich.... Anawajazaaaa.
LUQMAN: Mimi nilitaka Kamusoko anijibu swali moja tu, je, tulimkosea nini kipindi tukiishi mjini ‘Daslam’ kama ndugu? Kama aliyemuudhi ni Zahera kumwacha, si angetafuta namna ya ‘kudili’ naye kuliko kutubebesha msala sisi wote? Namdai Kamusoko!
LEVY: Watu kama Kamusoko si ajabu hakutaka kuondoka Bongo. Na huenda alikuwa na kidem cha Bongo Movie. Papaa Zahera kumtema kulimkera sana. Si ajabu angecheza hata bure.
LUQMAN: Sasa si angesema? Au kama ni hasira za Wema kuwa kimbaumbau kilichomzuia kufungua mdomo ni kipi? Kama alikuwa anamtaka Sarah wa Harmonize lakini Harmonize kamuoa jumla si angefunguka tu? Kamusoko ameingia kwenye orodha ya watu makatili 2019.
LEVY: Zahera naye ndo walewale. Anawabagaza sana Yanga. Kamusoko hakuwa wa kuachwa. Mtu kajifunza Kiswahili vizuri unamuacha aende Ndola kweli? Nadhani Kamusoko ndo mgeni pekee aliyejifunza haraka kiswahili. Huenda alitaka akistaafu soka ahamie Bongo Movie.
LUQMAN: Kamusoko ana kichwa chepesi sana kuzungumza Kiswahili. Huwezi kumfananisha na Nyoshi El-Sadat. Miaka 25 yupo Bongo lakini Kiswahili hajui. Ni dharau au ubongo wake una vitamini za Shilole? Maana Shilole naye mpaka British Council wamedunda.
LEVY: Nyoshi ‘alipataga’ dem mkali mwaka 1989 pale Magomeni Mikumi, kwa sababu ya kuongea vile. Ndo maana hataki kubadilika akidhani ndo ‘katalogi’. Na hao madem ambao wanadata na mtu anayeongea neno ‘Njo vile’ badala ya ‘Ndo vile’. Ujue ni dem wa kibwege kama mabwege wengine. Nyoshi yupo tangu 1983-84 mpaka leo eti hawezi kunyoosha Kswahili. Ndala Kasheba na King Kiki walikuja mwaka 1975 lakini 1976 wakatoa ngoma kama ‘Marashi ya Pemba’ humo Kiswahili kimenyooooka safi. Huyo Nyoshi anatufanya sisi mabwege.
LUQMAN: Labda wewe Nyoshi ndiye anakufanya bwege, mimi hanipati. Akianza kuongea tu naziba masikio. Christian Bella wa juzi anaongea Kiswahili kimenyooka kama kimechongwa na rula, Nyoshi wa miaka na miaka anajifanya lafudhi ya Kikongomani ndio ujiko mjini.
LEVY: Makambo hata mwaka hakumaliza, lakini alikuwa anabonga kiswahili safi na kina Anko Ngassa. Tshishimbi yule pale anatwanga kiswahili safi. Hata huyu nanii huyu nani mnamuita nani huyu... Mc nanii... Mc nani sijui... Naye ni Mkongo lakini anatwanga Kiswahili mpaka amekuwa Mc wa shughuli nyingi mjini na kaja mwaka juzi tu. Nyoshi atawashikia akili mabwege wa Kino na madem wa Mwananyamala huko.
LUQMAN: MC Pilipili sio Mkongomani, ni Mgogo wa Dodoma, usimsingizie yule janki kisa alilia kumvisha pete mchumba wake.
LEVY: Hakuna Mgogo wa vile wewe msikilize vizuri kiswahili chake. Acha kufananisha Wagogo na vitu vya ajabu. Kumbuka hata suti yake siku ya harusi yake. Mgogo gani anavaa suti ya pink?
LUQMAN: Kuongea kikogomani si ndio fasheni ya wengine, umesahau Jose Mara kuna kipindi alipenda ajulikane ni Mkongomani?
LEVY: Jose Mara bana. Yule naye nadhani alikuwa anashuhudia kina Patcho Mwambo Tajiri, wanavyong’oa totoz kali akajua kuongea kidwanzi vile ndo mizuka. Kumbe madem wenyewe wanaowabeba ndo wale wa usoni fanta mwilini koka. Yaani viganja kama mahindi ya kuchoma halafu usoni kama binzari. Hao ndo madem wa Wakongo.
LUQMAN: Unawaonea wivu Wakongomani, Daktari?
LEVY: Yaani niwaonee wivu watu ambao tunawaajiri kwenye bendi, timu zetu za soka mpaka kwenye saluni za kike? Kwa hiyo unataka na mimi niwe msusi au? Naona umeanza kunivunjia heshima kiaina. Next time zingatia kitu kabla ya kuropoka. Babaako Zahera tumemfungia mechi tatu kwa vipensi vyake.
LUQMAN: Hivi Hamorapa na yeye ni Mkongomani?
LEVY: Ndo walewale hata yule Steve Yanga naye anajifanya Mmanyema ila ukweli ni Mkongo yule. Tatizo lako ubishi ni jadi yako nikikuambia hata Kagere ni Mkongo utakataa...
LUQMAN: Dokta nikupe kazi ya ushenga?
LEVY: Kama ni kwa Nandy nitakuua. Kama kwa Wema au Hamisa  au Kajala au Wolper au Uwoya au Lulu poa tu. Maana Lulu naye sijui ndoa yake na Majizzo ina mapepo. Hivi ndoa ya Lulu inasubiri daftari la mpigakura?
LUQMAN: Kuna kitu Majizzo na Lulu hawataki kutwambia, nataka wewe ndio uwe mshenga ili tumalize kesi.
LEVY: Unanipa kazi ambayo naikataa kabla sijajua faida yake. Kwanza tunaotamani Lulu na Majizzo watemane ili kale ’Kalulu’ tukabebe jumla jumla tunakomenti wapi? Maana Majizzo analeta pozi za kindezi sana. Sasa si atangaze kukatema watu turuke nako juu kwa juu na kukaoa bila kusubiri radhi ya wazazi?
LUQMAN: Uchawi kweli upo. Yaani mtu katoa mpaka mahari, wewe unaombea watemane ili uchukue jumla. Ila nasisitiza, Lulu na Majay wana kitu hawataki kutwambia
LEVY: Hamna kitu chochote zaidi ya dua zetu tunaotaka wasioane. Kwa taarifa yako kale ‘Kalulu’ kanatamaniwa na mabaharia kibao. Kuna masista duu kibao wanawaza mkwanja wa Majizzo. Yaani kuna kundi la madem wa mjini linakesha likiombea Majizzo asimuoe Lulu ili waolewe wao. Kuna kundi la mabaharia kama mimi tunaombea Lulu asiolewe na Majizzo ili tumuoe sisi. Kifupi: “Dua za mabaharia zinakwamisha ndoa ya Lulu na Majizzo.”